Friday, February 17, 2017

Wabunge wazuiliwa kukutana na mfalme wa Rwenzururu Uganda

Wabunge kutoka Kasese, magharibi mwa Uganda , wanasema wamezuiliwa na vyombo vya usalama kukutana na mfalme wa Rwenzururu, Wesley Mumbere, licha ya mfalme huyo kuachiliwa kwa dhamana.
Wabunge hao ambao wote ni kutoka chama cha upinzani cha FDC, wanasema kuwa ni kama ambaye mkubwa wao yuko katika kizuizi cha nyumbani.


Kulingana na mwandishi wetu wa Kampala Siraj Kalyango wabunge wanne kutoka Kasese, Winfred Kiiza, Harlod Muhindi, William Nzoghu na Robert Muhindo wamelalamika kuwa mfalme wao anadhalilishwa.

Mfalme Mumbere amekuwa korokoroni tangu mwaka jana kwa sababu zinazohusika na uchochezi.

Serikali ilimfungulia mashtaka kadhaa ikiwemo ya mauaji, wizi na ugaidi baada ya kumkamata kufuatia makabiliano ya risasi kati ya maafisa wa usalama dhidi ya walinzi wa mfalme ambao serikali ilidai walikuwa wanajihusisha na visa visivyo sawa.

Febuari 6 mwaka huu mahakama ya juu ya mjini Jinja ilimuachilia Mumbere kwa dhamana ya polisi ya shilling za Uganda millioni 100 sawa na dola za Marekani 27,894, na wabunge hao ndio wadhamini wake.

Pia mfalme huyo aliamriwa kuwa kila baada ya muda fulani itambidi kurudi mahakamani.
Jumatatu anatakiwa kufanya hivyo na sasa yuko nyumbani kwake hapa mjini Kampala.

No comments:

Post a Comment