Mbowe jana alisababisha
taharuki katika kikao cha
Bunge baada ya kuzusha
tuhuma za rushwa kwa
wabunge wa CCM katika
kipindi cha maswali na
majibu na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa.
Ingawa swali lake hilo lenye
tuhuma lilizuiwa kujibiwa na
Naibu Spika, Dk Tulia Akson
kwa kuwa halikuwa swali la
kisera, hoja iliibuliwa tena
na wabunge wengine wakati
wa kuingia kipindi cha
majadiliano, kama
miongozo.
Mbowe katika swali lake
kwa Waziri Mkuu alituhumu
wabunge wa CCM, kupewa
rushwa ya Sh milioni 10 kila
mmoja na serikali ya chama
hicho ili kuupitisha
Muswada wa Huduma za
Habari unaowasilishwa
bungeni leo.
Aidha alidai rushwa hiyo, pia
imetolewa kupitisha Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa
mwaka 2017/18. Pamoja na
tuhuma hizo kutojibiwa na
Waziri Mkuu kutokana na
muundo wa maswali ya
papo kwa hapo kugusa sera,
Mbunge wa Momba, David
Silinde (Chadema) aliomba
mwongozo wa Spika huku
akitaka kuundwe Tume Huru
ya Kimahakama ya Bunge,
kuchunguza tuhuma hizo.
Naye Mbunge wa Chemba,
Juma Nkamia (CCM)
alisimama na kuomba
mwongozo, na kumtaka
Mbowe athibitishe tuhuma
hizo au achukuliwe hatua.
Nkamia alisema yeye akiwa
Mbunge wa CCM, hajapata
rushwa hiyo wala hakuiona
na kuhoji kwa nini Mbowe
ahoji wakati yeye si Mdhibiti
na Mkaguzi wa Hesabu za
Serikali (CAG), hivyo akitaka
Mbowe athibitishe tuhuma
hizo na akishindwa, alitaka
mwongozo ni hatua gani
Bunge itamchukulia.
Akijibu hoja zote hizo za
wabunge, Naibu Spika
alimtaka Mbowe kupeleka
tuhuma zake kwa vyombo
husika ili vichukuliwe hatua
stahiki.
Akifafanua zaidi, Naibu
Spika katika majibu yake ya
miongozo hiyo alisema
:“Wabunge tuwe makini,
ukisema kuna rushwa ujue
kuna vyombo vyake
maalumu vya kushughulikia
hilo, Bunge haliwezi
kusikiliza kesi hizo, Bunge
na Waziri Mkuu hawana
mamlaka kwa mambo
yasiyohusiana nayo,
nashauri suala hilo lipelekwe
kwenye vyombo husika.”
Kuhusu mwongozo wa
Nkamia, alisema kwamba
hatomtaka Mbowe
athibitishe kwani alimzuia
kuliongelea, lakini mwenye
uthibitisho apeleke kwenye
chombo kinachohusika na
rushwa ili kifanye kazi yake.
Mbowe aitisha mkutano
Baada ya tafrani hiyo
kuzuka bungeni na
kumalizwa na Naibu Spika
kwa kutoruhusu mjadala
wake, Mbowe aliitisha
mkutano na waandishi wa
habari katika ukumbi wa
Idara ya Habari na
Mawasiliano wa Bunge mjini
hapa, akiwa na Mnadhimu
wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Tundu Lissu na
viongozi wengine wa Chama
cha Wananchi (CUF).
Katika mkutano huo, Mbowe
alimtaka Rais Magufuli
kumtumbua Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa kwa kile
alichoeleza kuwa yeye
(Majaliwa) pamoja na
Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana
walihusika kutoa kwa
wabunge hao wa CCM 272
fedha hizo.
Alisema pia kuwa,
wanamuandikia barua Rais
kutaka aunde Tume ya
Kimahakama ya Uchunguzi,
kuchunguza suala hilo kwa
kuwa linawahusu wabunge,
na Bunge haliwezi
kujichunguza lenyewe.
Akifafanua kuhusu fedha
hizo, Mbowe alisema taarifa
walizonazo, zinathibitisha
kuwa katika kikao cha
wabunge wa CCM cha
Oktoba 25, mwaka huu,
Majaliwa na Kinana
waligawa fedha Sh milioni
10 kwa kila mbunge wa
CCM ili kuwapooza kuhusu
hali ya mdororo wa uchumi.
Alisema pia kuwa fedha
hizo, zilizoanza kutolewa
Oktoba 26, zililenga pia
kuwashawishi wabunge hao
wa CCM, kupitisha Muswada
wa Huduma za Habari wa
mwaka 2016 na Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa
mwaka 2017/18, ambao
mapendekezo yake
yamewasilishwa bungeni.
Mbowe alisema tuhuma hizo
ni nzito na Bunge haliwezi
kujichunguza lenyewe, hivyo
ni lazima iundwe tume huru
ya kimahakama kuchunguza
jambo hilo. Mbowe alisema
ushahidi wa kutosha wanao
na watautoa mbele ya tume
hiyo.
Mbowe alisema
walimshangaa Naibu Spika,
Dk Akson kwa kuwazuia
kutoa ushahidi ndani ya
Bunge, kama
walivyoombewa mwongozo
na Nkamia. Alieleza kuwa
hiyo ni mara ya kwanza kwa
upinzani, kuzuiwa kutoa
ushahidi kwa jambo,
ambapo linaonekana kama
ni uongo.
Lisu naye azungumza
Kwa upande wake, Lissu
alisema watamuandikia Rais
Magufuli barua rasmi
kueleza kilichofanywa na
viongozi wake, na kumtaka
achukue hatua kuhusu suala
hilo.
“Magufuli amejinadi yeye
anapambana na ufisadi,
mtihani wa pili aufanye na
aufaulu ni huu. Magufuli
amtumbue Kassim Majaliwa
kutoka kwenye nafasi hiyo
ya uwaziri mkuu,” alisema
Lissu.
Lissu alisema Sheria ya
Tume za Uchunguzi, inampa
Rais mamlaka ya kuunda
tume ya uchunguzi kwenye
jambo kubwa na muhimu,
linalohusu mambo ya umma.
“Katika barua hiyo
tunamgusia Tulia Ackson.
Kwa maoni yangu kisheria,
kiongozi wa kuteuliwa
anaondolewa na mamlaka
ya uteuzi, Rais amuondoe
huyu mama bungeni, hafai,”
alisema Lissu.
Viongozi wa CUF waliokuwa
katika mkutano huo ni
pamoja na Mbunge wa Viti
Maalum, Riziki Mngwali.
Awali, ndani ya Bunge
baada ya Naibu Spika
kuzuia swali hilo kwa kuwa
si la kisera, Mbowe akinukuu
Sheria ya Maadili ya
Utumishi wa Umma ya
mwaka 1995 na Sheria ya
Rushwa ya mwaka 2007,
alisema masuala ya rushwa
ni ya kisera.
Hata hivyo, Dk Akson
alimtaka Mbowe kuheshimu
kiti na kanuni, na kusisitiza
kuwa, yeye (Naibu Spika)
anaongozwa kwa kanuni na
kanuni zinaeleza kuwa swali
hilo si la kisera.
Friday, November 4, 2016
Majibu ya Mbowe kuhusu tuhuma za wabunge wa ccm
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment