Sunday, September 20, 2015

Kubandika matokeo ya urais vituoni kumechelewa

Mwenyekiti wa tume ya Taifa ya Uchaguzi,Damian
Mwenyekiti wa tume ya Taifa ya Uchaguzi,Damian Lubuva. 
Kwa namna ambavyo uamuzi wa kubandika matokeo ya kura za urais katika vituo vya kupigia kura umepokewa na wananchi, ni dhahiri kuwa huo ni uamuzi uliochelewa na ulikuwa unasubiriwa na wengi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) juzi ilitangaza kuwa kuanzia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, matokeo ya kura za urais yatakuwa yanabandikwa kwenye vituo vya kupigia kura sambamba na yale ya ubunge na udiwani, hatua ambayo imepongezwa na wengi.
Uamuzi huo wa Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva ulitolewa katika mkutano wa viongozi wa dini, baada ya viongozi hao kueleza wasiwasi wao katika uchaguzi huu, ikwamo kura za urais pekee kutobandikwa vituoni tofauti na zile za ubunge na udiwani.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, licha ya kubandikwa vituoni, utangazaji wa matokeo husika utafanyika kama kawaida katika kila ngazi, ya udiwani kwenye kata, ubunge wilayani, lakini matokeo ya jumla ya urais yatatangazwa na makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Pamoja na kuwaondolea wasiwasi wananchi kuhusu usalama wa kura zao, mwenyekiti huyo wa NEC aliwahi kukaririwa na gazeti hili akisema ,“Hakutakuwa na nafasi ya kuandaa vijana kulinda kura kwa sababu kura zote zitahesabiwa na kubandikwa huko.”
Kwa mtazamo wa Jaji Lubuva, matokeo hayo yakibandikwa vituoni, kila mtu atajua diwani kapata kura ngapi, mbunge na hata rais aliyemchagua. Itakuwa tofauti na zamani ambapo kura zilikuwa zinasafirishwa na kuhesabiwa wilayani ambako watu wengine walidhani matokeo halisi yanabadilishwa.
Uamuzi huu tunaona ulikuwa wa lazima, ingawa umechelewa kuchukuliwa kwa kuwa malalamiko dhidi ya matokeo ya uchaguzi ni ya muda mrefu, na hakukuwa na juhudi zinazoonekana za kuyafanyia kazi.
Pamoja na kwamba kubandika matokeo ya urais vituoni hakuwezi kuwa kipimo pekee cha uchaguzi kuwa huru na haki, sisi tunaamini kwamba huo ni mwanzo mzuri wa kuelekea katika uwazi unaohitajika katika upigaji na kuhesabu kura.
Ni imani yetu pia kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaendelea kufanyia kazi maeneo mengine, ambayo bado yanalalamikiwa kama kitendo cha kura kupigwa kwa mtindo wa kawaida licha ya kuwapo daftari la wapigakura la kielektroniki pamoja na usafirishaji wa kura kutoka eneo moja kwenda jingine.
Matarajio ya wengi ni kwamba Serikali iendelee kufanya mabadiliko ya msingi kwenye Tume na kuiwezesha kuendesha uchaguzi ulio huru, haki na wazi kwa viwango vinavyohitajika.
Wakati Tume inaendelea kufanya yaliyo ndani ya uwezo wake, Serikali inatakiwa iendelee kuandaa mazingira ya kisheria yatakayowezesha uchaguzi kuwa huru na haki, ili kuhakikisha matokeo ya uchaguzi yanaendana na kura zilizopigwa na hivyo kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya msingi.
Katika mchakato wa Katiba Mpya yalikuwapo masuala yanayohusu uchaguzi na kwamba Katiba Iliyopendekezwa ilikuwa na kipengele cha Tume Huru ya Uchaguzi, endapo mchakato huo utaendelezwa, suala hilo na mengine yanayokusudia kuufanya uchaguzi kuwa wa haki na huru pia yazingatiwe
Kwa kutambua kuwa amani ni tunda la haki, tunaamini kwamba kitendo chochote cha kuchezea haki za wananchi katika masuala ya msingi, kama Uchaguzi Mkuu ni ishara ya wazi ya kucheza na amani na utulivu wa nchi.
Tunavishauri vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kila linalowezekana, kuhakikisha wadau wote wa uchaguzi kila mmoja anatimiza wajibu wake ili kuhakikisha Taifa linabaki salama.