Sunday, September 20, 2015

KABWE AISHIKA CCM KUHUSU UFISADI

Kiongozi wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, amesema ufisadi ni kansa inayoitaf
una nchi inayoendelea kupoteza nchi mabilioni ya shilingi.

Amesema taarifa za serikali zinaonyesha  asilimia 30 ya bajeti ya nchi inaishia kwenye mifuko ya watu binafsi na wananchi wakiendelea kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Alitoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati akimnadi mgombea ubunge wa Kibaha mjini Habibu Mchange, aliyezindua kampeni zake jana.


Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu ajenda ya ufisadi imefifia tofauti na uchaguzi wa mwaka 2010. “ Jambo la kushangaza ni kwamba ajenda ya ufisadi imefifia katika uchaguzi tofauti na mwaka 2010, haipaswi kuwa hivi kwani ufisadi ni kansa inayotafuna taifa letu.”

Aliongeza kuwa ni lazima kuendelea kupambana dhidi ya ufisadi ili kuhakikisha nchi  inamaliza umasikini na kujenga dola la maendeleo ( developmental state ).

Alisema kuwa hali ni mbaya katika maeneo mbalimbali ya nchi na kutoa mfano wa mkoa wa Tabora ambao wananchi wake wanalima Tumbaku lakini haina soko licha ya zao hilo kuzalishwa kwa wingi na kuwa chanzo cha mapato ya nchi kwa fedha za kigeni.

“Tabora  huzalisha tumbaku nyingi zaidi kuliko mikoa yote nchini na kuingiza mapato ya fedha za kigeni zaidi ya dola za Marekani milioni 315 mwaka 2014.

Hata hivyo asilimia 10 ya mapato haya huibwa na vyama vya ushirika kwa kushirikiana na baadhi ya mabenki yanayosambaza pembejeo za kilimo.

Ufisadi huu kwenye tumbaku hauzungumzwi ilhali ndio mustakabali wa wakulima wa tumbaku zaidi ya milioni moja katika mkoa wa Tabora,” alisema.

Akielezea namna ufisadi unavyotawala siku hadi siku, Zitto alisema kuwa mwezi uliopita (Agosti) serikali kupitia mfumo wa kuagiza mafuta kwa pamoja ilitoa zabuni kwa kampuni ya Augusta kutoka Switzerland na kwamba zabuni hiyo  ilipandishwa bei kwa thamani ya dola milioni 10 sawa na Sh. bilioni 20.

Alisema hali hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa mafuta kuendelea kupanda bei nchini wakati katika soko la dunia bei ikiwa imeshuka.

Aliongeza kuwa  mpaka sasa bado kampuni ya IPTL inauza umeme wa Shirika la Umeme (Tanesco) licha ya Bunge kuazimia kuwa mkataba wake uvunjwe, huku mtu  anayejiita mmiliki wa IPTL aliyetapeli nchi akiwa bado   hajakamatwa.

Akizungumzia vyama vinavyotaka kupata ridhaa ya kuongoza nchi mbali na ACT-Wazalendo, Zitto alisema vyama hivyo  vinatamka kauli nyepesi nyepesi kuhusu mapambano dhidi ya ufisadi.

Alisema ni wakati muafaka wa kuirejesha ajenda ya ufisadi kwenye kampeni za uchaguzi kwa kila chama kusema kitafanya nini na kwamba  ACT-Wazalendo wameweka kwenye ilani yao hatua watakazochukua kupambana na rushwa na ufisadi.

Aliainisha hatua hizo kuwa ni kuipa mamlaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ya kukamata na kuendesha mashtaka ya rushwa bila kusubiri kibali cha mwendesha mashitaka wa serikali, kuanzisha idara ya rushwa kubwa kubwa ambayo kazi yake itakuwa ni kupambana na ufisadi na kutunga sheria ya miiko ya uongozi ili kudhibiti rushwa kwenye sekta ya umma na siasa.

Alisema njia nyingine ni kwa mali za viongozi kuwekwa wazi na kukaguliwa na pale kwenye udanganyifu hatua kuchukuliwa ikiwemo kuvuliwa madaraka yao.

“Ni imani ya chama chetu kuwa ajenda ya ufisadi itajadiliwa kwa kina kwenye kampeni na hasa kwenye midahalo ya wagombea Urais na viongozi wa vyama, nawaomba wananchi wa Kibaha muichague ACT Wazalendo ili iweze kuendeleza vita dhidi ya ufisadi na kusafisha nchi yetu dhidi ya wala rushwa.

Naomba kura kwa Habib Mchange kama mbunge, madiwani wa ACT Wazalendo na mumchague mama Anna Mghwira kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Chagueni ACT Wazalendo ili kurejesha nchi yetu kwenye misingi,”alisema.

Kwa upande wake Mchange alisema amerejea kuwania ubunge wa Kibaha kuendeleza hatua aliyoiacha mwaka 2010 ya kupigania maslahi ya wana Kibaha.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment