Tuesday, July 7, 2015

SINGANO MESS AIBWAGA SIMBA

Ramadhan SinganoRamadhan Singano
 
KLABU ya Simba imepigwa mweleka katika vita na mshambuliaji wake, Ramadhan Singano ‘Messi’ kwenye mgogoro wao wa kimkataba uliodumu kwa takribani miezi mitatu.
Maamuzi ya mgogoro huo yametolewa jana mbele ya waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa na kusema Simba imeshindwa kutekeleza masharti ya mkataba.
Alisema kuwa awali waliuagiza uongozi wa klabu hiyo wakayafanyie kazi lakini hadi kikao cha jana kinakaa hakuna kilichotekelezwa.

“Awali TFF tulimwita Ramadhan Singano na uongozi wa Simba baada ya kuwasikiliza kila mmoja tukaagiza wakae meza moja lakini Simba hawakufanya hivyo na shauri hilo likalazimika kupelekwa kwenye Kamati ya Maadili, Sheria na Hadhi za Wachezaji na Maamuzi yametoka kuwa mchezaji Ramadhan Singano yupo huru kuanzia leo,” alisema Mwesigwa. Mwesigwa alisema Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, iliwakilishwa na Mwenyekiti Wakili Richard Sinamtwa na mchezaji Ramadhan Singano alikuwa amefuatana na Mwenyekiti wa Sputanza, Mussa Kisoky na Katibu Said George wakati Simba iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collin Frisch na Mkurugenzi wa Wanachama wa TFF, Eliud Mvella. Kikao hicho kilichukua karibu saa tano kumalizika huku kila upande ukilazimika kutolewa nje wakati upande mwingine ukihojiwa mwishoni upande wa Simba ulitoka ukiwa umenyong’onyea wakati Kisoky na wenzake wakitoka `meno’ nje huku wakikumbatiana na kuwadokeza waandishi: “Tumeshinda kijana yupo huru ila sisi si wasemaji subirini TFF watatoa taarifa kamili.” Baadaye gazeti hili lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe na kuweka wazi kuwa hawajaridhishwa na maamuzi ya kamati hiyo hivyo watakutana ili kujua hatua zaidi za kuchukua ikiwezekana watakata rufaa kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Mambo ya Michezo (CAS)ili kudai haki yao. “Tuliwasilisha ushahidi wote mbele ya Kamati, tumeonesha mshahara wake ulikuwa kiasi gani na tumeonyesha kwa nini alikuwa anapewa laki moja (100,000) zaidi. Lengo lilikuwa akalipie kodi ya nyumba, lakini bado hatukueleweka. Tunaamini hapa si mwisho, vipo vyombo vingine ambavyo vitatupa haki yetu, tunakwenda kukutana kuangalia uwezekano wa kulipeleka suala hili huko.” Kamati ya Sinamtwa imejiridhisha Messi hakuwahi kupewa nyumba ya kuishi na Simba jambo ambalo ni kinyume cha mkataba baina yake na klabu hiyo, hivyo imemevunja rasmi mkataba wake na kusema yupo huru kusajiliwa na klabu yoyote. Messi alikuwa anailalamikia Simba kupeleka TFF mkataba wa miaka mitatu wakati yeye alikuwa na mkataba wa miaka miwili na Simba, jambo lililoleta utata hadi Sputanza kuamua kumsaidia na hatimaye Messi kushinda. Messi alisajiliwa Simba miaka minne iliyopita kwenye Simba B na baadae kuingizwa kwenye kikosi A baada ya uwezo wake kuwaridhisha makocha mbalimbali ambao wamekuwa wakiifundisha Simba kwa nyakati tofauti.

No comments:

Post a Comment