Waziri wa Fedha, Saada Mkuya leo atawasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 ambayo wachambuzi wameielezea kuwa itakuwa na unafuu kwa wananchi kutokana na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Wakati wachambuzi wakiielezea kuwa ni bajeti ya
uchaguzi, wabunge waliozungumza na Mwananchi jana walisema hawatarajii
kitu kipya kwa kuwa kila mara wamekuwa wakiipitisha kwa makofi, lakini
utekelezaji unakuwa mdogo na sababu zimekuwa ni ukosefu wa fedha.
Bajeti hiyo ya Sh22.4 trilioni, ongezeko la
asilimia 16 kulinganisha na bajeti ya mwaka 2014/15 ya Sh19.6 trilioni,
inatarajiwa kuboreshwa kwenye maeneo kadhaa baada ya wabunge kuchachamaa
wakati wa uwasilishaji wa bajeti za wizara mbalimbali.
Wabunge waligeuka mbogo wakati wa upitishaji wa
bajeti za wizara hasa kutokana na Serikali kushindwa kupeleka fedha za
miradi ya maendeleo kwa angalau asilimia 50 ya fedha zilizotengwa kwenye
bajeti inayomalizika, na wakati mwingine ilibidi Waziri Mkuya asimame
kutoa ahadi kuwa masuala hayo yangepelekwa kwenye Kamati ya Bajeti
kuboreshwa.
Hii ni mara ya pili kwa Waziri Mkuya kuwasilisha
bajeti baada ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka jana
alipowasilisha ya mwaka unaomalizika Juni 30.
Akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa bajeti kwa
mwaka wa fedha 2015/16 unaoanza Julai Mosi, Mkuya alisema Serikali
imepania kupunguza utegemezi wa fedha kutoka kwa wahisani na wafadhili
kutoka asilimia 14.8 hadi asilimia 8.4 na kwamba itajikita zaidi katika
kukusanya kodi kwa kuhimiza matumizi ya vifaa vya kielektroniki.
Wachambuzi walihojiwa na Mwananchi jana walielezea
bajeti hiyo kuwa italenga zaidi kutoa matumaini kwa wananchi, lakini
itakuwa vigumu kutekelezeka.
“Kwa mfano, kupunguza utegemezi kwa wahisani ni
tumaini zuri, lakini shaka ni malimbikizo ya madeni kwa makandarasi,
walimu na taasisi nyingine zinazojiendesha. Tatizo jingine ni bajeti
kidogo iliyotengwa kwa maendeleo,” alisema Profesa Humphrey Moshi kutoka
Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT), Ezekiah Oluoch alisema bajeti hiyo haina matumaini kwa watumishi
wa umma hususani walimu nchini kutokana na mambo mengi kutoonekana.
“Niliangalia kwa umakini bajeti ya elimu na
kuichambua, lakini mambo mengi ya msingi hayajaonekana. Mfano fungu la
kulipa madeni ya walimu wastani wa Sh20 bilioni halipo, bajeti ya
kuanzisha Tume ya Utumishi wa Walimu hakuna.”
Mbali na kupunguza utegemezi kwa nchi wahisani na
wafadhili, Serikali pia ilitangaza nafuu kubwa katika ada na kodi
mbalimbali za ardhi, baada ya kuzishusha kwa wastani wa asilimia 50,
jambo linaloonekana kuwa la kuwapa matumaini wananchi wakati huu wa
kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Katika taarifa ya mwelekeo wa bajeti kwa mwaka wa
fedha 2015/16 unaoanza Julai Mosi, Mkuya alitangaza vipaumbele vyake,
ikiwamo kugharamia uchaguzi mkuu, kukamilisha miradi inayoendelea,
kuweka msukumo maalumu kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini na
kuimarisha rasilimali watu.

No comments:
Post a Comment