Kwa mara kwanza Bajeti ya 2015/16, ambayo ni ya mwisho ya
Serikali ya Awamu ya Nne, haijaongeza kodi katika bidhaa za pombe na
sigara, badala yake imeendelea kupandisha kodi katika mafuta huku
ikiminya uingizaji wa bidhaa nchini kwa ajili ya kulinda viwanda na
wazalishaji wa ndani na kuongeza ajira.
Pia, bajeti hiyo ya mwisho kwa utawala wa Rais
Jakaya Kikwete imeweka kipaumbele katika kugharamia Uchaguzi Mkuu,
kuweka msukumo maalum kwenye miradi ya umeme vijijini, maji vijijini,
kukamilisha miradi ya kimkakati inayoendelea pamoja na kuwekeza kwenye
rasilimali watu.
Bajeti hiyo imeeleza mikakati mbalimbali ya
ukusanyaji mapato kwa kufanya mageuzi kwenye mfumo wa kodi, kudhibiti
mianya ya matumizi ya fedha za Serikali, kupunguza misamaha ya kodi,
kupunguza kero za wastaafu kwa kuwaongezea mafao ya mwezi kutoka
Sh50,000 hadi Sh85,000, kupunguza Kodi ya Malipo ya Kadri ya Mapato
(Paye) kwa asilimia moja na kuanzisha mafao ya kila mwezi kwa wazee.
Akiwasilisha bajeti hiyo ya mwaka wa fedha wa
2015/16, Waziri Mkuya alipendekeza mabadiliko ya sheria mbalimbali
zitakazosaidia kupunguza na kuongeza kodi zitazoisadia Serikali kuongeza
mapato ili iweze kufanikisha utekeleji wa bajeti ya Sh22.5 trilioni.
Waziri Mkuya aliliomba bunge liridhie mabadiliko
katika Sheria ya Sheria ya Mafuta ya Petroli Sura namba 392 ili kuongeza
tozo ya mafuta ya petroli na dizeli kutoka Sh50 hadi Sh100.
Pia, tozo ya mafuta ya taa imependekezwa kuongezwa
kutoka Sh50 hadi Sh150 ikiwa ni moja ya njia ya kupunguza uwezekano wa
uchakachuaji.
“Hatua ya kuongeza Tozo ya Mafuta ya Petroli
inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh139.78 bilioni
na fedha zote zitaelekezwa katika mfuko wa Rea kwa ajili ya utekelezaji
wa mradi wa usambazaji umeme vijijini,” alisema Mkuya huku baadhi ya
wabunge wakionyesha kupinga.
Pia, Mkuya alipendekeza mabadiliko katika Sheria
Tozo za Mafuta na Barabara namba 220 ili kuongeza tozo katika mafuta ya
Dizeli, Petroli na kwa Sh50 hadi kufikia Sh313.
Alisema hatua hiyo ya kuongeza tozo hiyo pia
itaongeza mapato kwa takribani Sh136.4 bilioni ambayo alisema
yataelekezwa katika mradi wa kusambaza umeme vijijini wa Rea.
Pamoja na maumivu hayo, Mkuya alipendekeza Waziri
wa Fedha apatiwe mamlaka ya kusamehe Tozo ya Mafuta ya Petroli kwenye
miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili na yenye mikataba
isiyohusisha utozaji wa tozo hiyo ili kuondoa usumbufu na ucheleweshaji
katika utekelezaji wake.
Katika jitihada za kulinda viwanda vya ndani na
kuongeza ajira, Serikali inapendeleza mabadiliko ya Sheria za Kodi ya
Mapato namba 332, Sheria ya mauzo ya nje namba 196, Sheria ya Forodha ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 na Sheria ya Uwekezaji
Tanzania Sura 196.
Waziri Mkuya alibainisha kuwa ili kumpunguzia
mzigo mfanyakazi wamependekeza kupunguza kiwango cha chini cha kutoza
kodi ya mapato ya ajira kutoka asilimia 12 hadi asilimia 11 akibainisha
ni dhamira ya Serikali tangu mwaka mwaka 2006/07 kodi hiyo ilipokuwa
asilimia 18.5.

No comments:
Post a Comment