MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliyevuliwa
nyadhifa zote za uongozi kwa madai ya usaliti, amekemea vurugu
zinazofanywa na baadhi ya wanachama wanaopinga uamuzi wa chama.
Zitto, amewataka wanachama wa CHADEMA kuwa watulivu na kuwaheshimu
viongozi wa kitaifa wanaofanya kazi ya ujenzi wa chama mikoani.
Tangu Zitto avuliwe uongozi, baadhi ya wanachama wa CHADEMA wamekuwa
wakifanya vurugu kwenye mikutano inayofanywa na Katibu Mkuu wa CHADEMA,
Dk. Willibrod Slaa, anayefanya ziara mkoani Kigoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
mwanasheria wa mbunge huyo, Albert Msando, alisema Zitto hahusiki na
vurugu zinazoendelea katika ziara za Dk. Slaa.
Alisema Zitto anataka utulivu uwepo ndani ya chama kwakuwa anaamini
sakata la kuvuliwa uongozi litamalizika bila kukiathiri chama.
“Zitto anasema amesikitishwa na matukio yanayotokea katika ziara ya
Dk. Slaa ambayo sasa yamekuwa fujo zinazoendana na kurushiwa mawe,
hahusiki na vurugu hizo,” alisema Msando kwa niaba ya Zitto.
Msando alisema licha ya vurugu hizo kuhusishwa na Zitto, kiongozi
huyo ameweka wazi kuwa anaamini utulivu na heshima utakivusha chama
katika kipindi hiki.
Zitto akata rufaa
Msando alisema Zitto amemuandikia barua Katibu Mkuu wa CHADEMA,
kuelezea nia ya kukata rufaa kwa Baraza Kuu la chama kupinga namna
Kamati Kuu ilivyomvua nafasi za uongozi.
Alisema licha ya Zitto kufuata taratibu za chama kwa juzi kuwasilisha
utetezi wake kutaka asivuliwe uanachama, pia ameamua kukata rufaa
kupinga kuvuliwa vyeo alivyokuwanavyo.
Alizitaja sababu za kupinga uamuzi huo kuwa ni kukiukwa kwa utaratibu wa kuchukua hatua za kinidhamu.
Msando alisema kifungu cha kanuni ya Katiba ya CHADEMA 6:5:6
kinaeleza kuwa kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu bila
kwanza kupewa mashitaka yake kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa
nafasi ya kujibu kwa maandishi.
Alisema kanuni ya uendeshaji 6.5.2 (a), (b), (c) na (d) kama
ilivyorekebishwa Januari 2013 inasema: “Kwa mujibu wa ibara ya 5.4.3 na
5.4.4 ya katiba mwanachama yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama
kuonywa ama kuachishwa ama kufukuzwa uanachama bila kwanza; a)
Kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika
muda usiopungua wiki mbili.
“b) Kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kinachohusika, c)
Mwanachama atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao mnamo wiki mbili
baada ya kusikilizwa, d) Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura
bila kuzingatia utaratibu (b), (c) hapo juu kama itaona maslahi ya chama
kwa ujumla yanaweza kuathiriwa isipokuwa mwanachama au kiongozi
anayelalamikiwa atalazimika kuitwa kwenye kikao husika.”
Aliongeza kuwa Novemba 26 uongozi wa chama ulifanya mkutano na
waandishi wa habari na kueleza kuwa marekebisho hayo ya kanuni ya mwaka
2013 ndiyo utaratibu uliofuatwa katika kuwavua uongozi Zitto na wenzake,
na kwamba wakili Msando alidanganywa juu ya vifungu hivyo kwa kuwa
vilishabadilishwa.
Alisema hatua ya dharura iliyochukuliwa na Kamati Kuu haikugusa
kipengele (a) cha kanuni kinachoeleza kuwa kama Kamati Kuu itachukua
hatua ya dharura kwa mujibu wa kipengele (d), bado kipengele (a) ni
lazima kifuatwe na kwamba inatamka wazi sharti la kiongozi kupewa
mashitaka kwa maandishi na kupewa nafasi ya kujibu kwa maandishi.
“Hii ni haki ya msingi kwa kila utawala au uongozi. Zitto Zuberi
Kabwe hakupewa mashitaka yake aliyakuta ndani ya kikao baada ya kupewa
taarifa kwa ujumbe wa simu (text message au sms),” alisema Msando.
Msando alisema kwa uzito wa makosa hayo yaliyosababisha kuvuliwa
uongozi na kwa kuangalia athari zake kwa Zitto binafsi na chama kwa
ujumla, Kamati Kuu ilitakiwa kujiridhisha kwamba kanuni za uendeshaji na
katiba zinafuatwa.
Aliongeza kuwa utaratibu uliotumika kumvua Zitto na Dk. Kitila
madaraka unaendana na utaratibu uliotumika kumvua uongozi Samson
Mwigamba aliyekuwa kiongozi wa chama hicho Mkoa wa Arusha.
Alisema hadi sasa mteja wake hajapokea taarifa rasmi ya maandishi kwa
mujibu wa kanuni za uendeshaji, zinazoonyesha kwamba ameshiriki kwenye
kuandaa na kusambaza waraka unaosemekana ni mkakati wa ushindi wenye
lengo la kupindua uongozi uliopo.
Msando aliongeza kuwa licha ya wahusaika wa waraka huo kusema kuwa
Zitto hahusiki, Kamati Kuu iliamua kumuadhibu kwa hisia kutokana na
urafiki wake na baadhi ya watuhumiwa.
Mwigamba aiburuza CHADEMA kwa msajili
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba,
aliyekuwepo kwenye mkutano huo, alisema amemuandikia barua Msajili wa
Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, akimuomba atoe muongozo
kuhusu mgogoro wa kikatiba uliopo ndani ya chama chao.
Alisema mwongozo huo unajikita kwenye kipengele kinachogusia ukomo wa uongozi kubadilishwa kinyume na utaratibu.
Mwigamba alisema Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2004 kipengele 5.3.2 (c)
kinasema kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na
kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa
kiongozi kwa muda usiozidi vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi
moja.
Alibainisha kuwa Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006 kipengele cha 6.3.2 (
c) inayozungumzia muda wa uongozi kinasomeka kuwa kiongozi aliyemaliza
muda wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena, mradi awe
anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi, huku akibainisha kuwa
sentensi kuhusu ukomo wa uongozi imeondolewa.
“Ni kweli kuwa marekebisho ya katiba yalifanyika mwaka 2006, lakini
hoja ya pili ya kubadili kipengele hicho haikuwepo na muhtasari
zinaonyesha wazi kuwa kulikuwa hakuna mjadala wa kipengele hicho au
kuhusu suala zima la ukomo wa uongozi,” alisema Mwigamba.
Alisema si kweli kwamba CHADEMA haijawahi kuwa na katiba ambayo ina
ukomo wa uongozi, na kwamba katiba ya 2006 haikuandikwa upya bali
marekebisho yalifanywa kwa baadhi ya vipengele huku kipengele 5.3.2 (c )
kikiwa hakijawahi kujadiliwa.
Ziara ya Dk. Slaa
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, jana aliendelea na ziara
yake katika Jimbo la Kigoma Mjini ambako alisema hawatokubali viongozi
na watendaji wa chama hicho wanaowekana mezani.
Dk. Slaa, alisema chama kimejiwekea utaratibu wa kuhakikisha kila
kiongozi atapatikana kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, akiwaagiza
viongozi wa kanda 10 za chama hicho kuhakikisha wanasimamia suala hilo
kama ilivyoagizwa kwenye waraka wa Katibu Mkuu namba 6.
Alisisitiza umuhimu wa chama hicho kufanya uchaguzi kuanzia ngazi ya
chini ambayo ni msingi kwa kila kitongoji au mtaa, huku kikijiandaa kuwa
na mabalozi wa nyumba 10.
Aidha, Dk, Slaa alisema kuwa suala la makada waliovuliwa nafasi zao za uongozi halijafika mwisho.
“Suala la Zitto na wenzake wawili wala sitalizungumzia kwa sababu
taratibu za chama kupitia vikao hazijakamilika. Lakini nitazungumzia
maneno ya upotoshwaji yanayoendelea kuhusu suala hili, yako kwenye
mitandao, yako vijiweni na wengine hawajui wanayapokea tu na kufikiri
ndiyo ukweli,” alisema.
No comments:
Post a Comment