
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la Katibu
wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda la kufanya
mapitio ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro wa kukataa
kumfutia kosa la uchochezi wakati yupo kwenye kifungo cha mwaka mmoja
nje.
Akitoa uamuzi huo jana, Jaji Rose Temba, alisema ombi hilo limekosa thamani katika jicho la sheria.
Jaji Temba alisema Oktoba mwaka huu, mawakili wa Ponda
walivyowasilisha ombi hilo kabla jalada halijapelekwa kwa Msajili wa
Mahakama Kuu Dar es Salaam alipata fursa ya kulipitia na kubaini
upungufu kwenye hati ya kiapo.
“Nilishangaa Desemba 2 mwaka huu, wakili wa Ponda, Juma Nassoro
alipinga kiapo hicho kilikuwa hakina dosari… binafsi nilipitia jalada na
kuona rekodi za mahakama haziko sahihi na zilirekebishwa kinyemela
baadae, kitendo hicho kinahesabika kama ni utovu wa nidhamu.
“Ukiukwaji huu hauwezi kuachwa hivi hivi bali vyombo
vinavyoshughulika na nidhamu kwa mawakili nchini viwachukulie hatua
mawakili wa Ponda,” alisema.
Akizungumzia hoja ya kiapo kuwa kina dosari, Jaji Temba alisema
anakubaliana na pingamizi la awali la upande wa Jamhuri lililowasilishwa
na Wakili Kiongozi wa Serikali, Bernad Kongora kuwa kiapo hakina tarehe
na baadae kilifanyiwa marekebisho kinyemela.
“Kwa dosari hiyo ya hati ya kiapo, mahakama inakubaliana na Wakili wa
Jamhuri, Kongola kuwa ombi la mapitio nalo limekosa thamani katika
jicho la sheria na kwa maana hiyo mahakama inakubaliana na pingamizi la
awali la upande wa Jamhuri kuwa kiapo kina upungufu,” alisema.
Desemba 2 mwaka huu, Kongora aliwasilisha pingamizi la awali akiomba
mahakama hiyo itupilie mbali ombi hilo kwa sababu hati ya kiapo ina
dosari.
Oktoba mwaka huu, Ponda aliwasilisha ombi hilo kupinga uamuzi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro kukataa kumfutia kosa la uchochezi
wakati yupo ndani ya kifungo cha mwaka mmoja nje ambacho kilimtaka
asitende makosa na awe raia mwema.
Sheikh Ponda anadaiwa kutenda kosa hilo Agosti mwaka huu mkoani Morogoro.
No comments:
Post a Comment