Wednesday, December 11, 2013

HII NI HALI HALISI KUMUAGA MANDELA


Mazishi ya Mandela


VIUNGA vya Jiji la Pretoria nchini Afrika Kusini, jana viligubikwa na umati mkubwa wa watu waliokusanyika katika jengo la Umoja kwa ajili ya kuuaga mwili wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Nelson Mandela.
Mwili wa Mandela aliyefariki wiki iliyopita, ulichukuliwa kwa msafara kutoka chumba cha maiti cha hospitali ya jeshi ulikokuwa umehifadhiwa hadi kwenye jengo la Muungano ambalo mwaka 1994, alilitumia wakati akila kiapo cha kuwa rais wa nchi hiyo.
Helikopta na pikipiki za polisi zilikuwa zikilisindikiza gari maalumu lililobeba jeneza la Mandela, ambalo lilifunikwa kwa bendera ya Afrika Kusini kutoka hospitalini.
Gari hilo lilipita mitaani kwa mwendo wa taratibu ambako kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliojipanga kando ya barabara lilipopitishwa jeneza kama ishara ya kutoa heshima za mwisho.
Msafara ulipita katika mitaa huku baadhi ya raia wakikimbia pembeni kwa lengo la kuona jeneza la muasisi wa taifa hilo aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95.
Wananchi, wakuu wa nchi walioalikwa na wageni wengine wa kimataifa watapata nafasi ya kutoa heshima za mwisho kwenye mwili wa Mandela atakayezikwa Jumapili nyumbani kwake katika Kijiji Qunu katika Jimbo la Cape Mashariki.
Kwa mujibu wa mashirika ya habari nchini humo, familia ya Mandela, ilikuwa ya kwanza kutoa heshima za mwisho ambapo vilio na simanzi vilitawala katika majengo ya Umoja.
Jeneza la Mandela liliwekwa kwenye jukwaa ndani ya majengo hayo.
Katika kudumisha tamaduni za Kiafrika na kulienzi vazi la batiki ambalo Mandela alipenda kuvaa enzi za uhai wake, mwili wake ulikuwa umevikwa shati la batiki kutoka nchini Indonesia, lililoonekana kupitia kioo cha jeneza alimohifadhiwa.
Mjane wake Graรงa Machel alionekana akiwa ameinamisha kichwa chini kwa huzuni akitembea hatua chache nyuma ya Rais Jacob Zuma baada kutoa heshima za mwisho kwenye jeneza la mumewe.
Mke wa zamani, Winnie Madikizela Mandela na binti zake ndiyo waliofuatia kutoa heshima zao kabla ya marais wa zamani Thabo Mbeki na Fredrick Wille de Klerk kutoa heshima zao.
Rais wa zamani wa Zambia, Kenneth Kaunda alikuwa wa kwanza katika kikosi cha viongozi wa Afrika kutoa heshima zao za mwisho akifuatiwa na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Goodluck Jonathan wa Nigeria na Ellen Sirleaf Johnson wa Liberia.
Usalama waimarishwa
Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa kila kona huku askari wa polisi na wale wa usalama barabarani wenye silaha wakiwa wamesambazwa katika kila kona ya  mji.
Maofisa wa polisi na askari walikuwa nje ya majengo ya Umoja, huku magari ya polisi, malori ya kijeshi, na mizinga yakiwa yamejipanga katika eneo hilo.
Helikopta nazo zilikuwa zikirandaranda huku na kule angani kuhakikisha waombolezaji wanatoa heshima zao katika usalama.
Picha zaruhusiwa
Maofisa wa usalama mjini Pretoria walilazimika kuruhusu waombolezaji kuchukua picha za kumbukumbu ya Mandela kwa kutumia simu za mkononi.
Awali ilizuiwa picha kupigwa kwa aina yoyote ile wakati wa kuuaga mwili huo.
Utaratibu wakera waombolezaji
Baadhi ya raia waliokusanyika kutoa heshima zao za mwisho kuanzia jana saa mbili asubuhi walionekana kukerwa na foleni kubwa iliyosababisha msongamano.
Waombolezaji hao waliitupia lawama kamati ya maandalizi ya mazishi kwa kushindwa kubuni utaratibu unaofaa.
Mmoja wa waombolezaji aliyejitambulisha kwa jina la Matema alinukuliwa na vyombo vya habari akihoji sababu zilizowafanya viongozi walichague eneo la Majengo ya Umoja.
Taarifa kutoka katika mashirika ya habari nchini humo zinaeleza kuwa nyakati za mchana, baadhi ya watu walikuwa wakilalamika kuhusu zoezi la utoaji wa heshima za mwisho linavyokwenda polepole.
“Mimi sijui jinsi mipango yetu ya serikali, lakini utaratibu huu foleni inaelekea kuleta kero na mkanyagano ambao unaweza kuleta  machafuko,” alisema Irvin Leset, mmoja wa waombolezaji.

No comments:

Post a Comment