Licha ya kupita miaka 40 tangu Uingereza ijiunge na Muungano wa
Ulaya (wakati huo jina lilikuwa Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya), bado
mabishano yangaliko miongoni mwa raia wa visiwa hivyo, kuhusu kero
ndani ya Muungano huo, na kama ni bora hivi sasa nchi hiyo ijitoe.
Hali hiyo imezifanya nchi nyingine shirika ndani
ya Muungano huo kulalamika kwamba Uingereza ni korofi, inazuia mwenendo
wa kuzidi kuiunganisha Ulaya itakayokuwa imara zaidi na huenda siku moja
ikawa na Serikali moja.
Januari mwaka huu Waziri Mkuu wa Uingereza, David
Cameron alitangaza kwamba huenda, baada ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka
2015, iwapo atashinda, huenda Waingereza wakatakiwa kupiga kura ya maoni
mwaka 2017 kama wanataka nchi yao ibakie ndani ya Muungano wa Ulaya.
Hata hivyo, bado kuna wabunge kutoka chama chake
cha Conservative walioonesha hawajatosheka tu na ahadi hiyo ya kiongozi
wao –Walitaka zaidi, na kumbinya aweke wazi kupitia sheria kwamba kura
hiyo ya maoni hakika itafanyika, na isitegmee chama chake kushinda
uchaguzi ujao au yeye kubakia madarakani hadi wakati huo.
Pia wala isitegemee matokeo ya mashauriano ambayo
Uingereza inataka yafanyike ili ijipatie masharti mapya yaliyo bora
kubakia katika Muungano huo.
Wiki iliyopita wabunge 130, wengi wao wakiwa
kutoka Chama cha Conservative ambao wanakerwa na mfumo wa Muungano wa
Ulaya na namna nchi yao inavyotendwa, waliwasilisha bungeni muswada
uliolaumu msimamo wa Serikali yao kuelekea Muungano huo.
Ilikuwa kama kumpiga kibao cha usoni Cameron. Mswada huo ulishindwa kupita bungeni, lakini ulitoa ishara muhimu ya kisiasa.
Ni wazi kwamba hisia za Waingereza wengi kupinga
nchi yao kubakia ndani ya Muungano wa Ulaya zinazidi, japokuwa wachache
kati yao ni kutokana na uzalendo kuliko kuangalia hali halisi ya mambo.
Mada juu ya werevu wa kuitisha kura ya maoni
inabakia katika vichwa vya habari, na hata katika chaguzi za karibuni za
Serikali za Mitaa chama cha Ukip, kinachotaka Uingereza itoke kutoka
Muungano wa Ulaya, kilifanikiwa kupata kura nyingi za kutoka wanachama
wa chama tawala cha Conservative.
Chama hicho cha Ukip katika uchaguzi ujao huenda
kikaweza kukipotezea ushindi chama cha Conservative, na kuacha njia wazi
kwa chama cha Labour kuingia madarakani. Wanachama wengi wa Chama cha
Conservative hivi sasa wanataka viongozi wao watamke wazi na bayana
kuhusu nchi yao kubakia ndani ya Muungano.
Kilichowaudhi wabunge hao waliowasilisha muswada
wao ni kwamba katika hotuba ya karibuni aliyoitoa Malkia bungeni- ambayo
ni programu ya Serikali kwa siku zijazo- hakujatajwa kwamba Serikali
itawasilisha rasimu ya sheria bungeni kuhusu kuitishwa kura ya maoni.
Kwa hakika Cameron asingepinga Serikali yake
kuwasilisha rasimu ya aina hiyo. Lakini ana tatizo. Nalo ni kwamba
Serikali yake ni ya mseto ambapo ndani yake kuna chama cha Liberal
Democratic kinachopinga au mara nyingine kutia na kutoa kuhusu suala la
kuitishwa kura ya maoni.
No comments:
Post a Comment