Wapiganaji 30 wa kundi la wanamgambo la Hezbollah wanaripotiwa kuuwawa
katika mapigano yaliyotokea katika mji wa Qusayr nchini Syria huku
wengine zaidi ya 70 wakijeruhiwa.
Duru za kuaminika zinasema wapiganaji wa Hezbollah wanaoshirikiana na
wanajeshi wa utawala wa Rais Bashar al Assad wamekuwa wakikabiliana na
waasi kwa wiki moja sasa katika eneo la Qusayr ambalo ni muhimu kwa
sababu inaunganisha Damscus na pwani ya nchi hiyo na pia iko mpakani na
Lebanon.
'Shirika la kutetea haki za binadamu nchini humo lenye makao
yake nchini Uingereza limesema karibu watu 55 wameuwawa katika mji huo
wengi wao wakiwa ni waasi mbali na wapiganaji wa Hezbollah na wanejeshi
wa serikali.
Kulingana na shirika hilo ambalo linategemea taarifa na
takwimu kutoka kwa wanaharakati,madaktari na wanasheria walioko nchini
humo kiasi ya watu 94,000 wameuwawa tangu mzozo wa Syria kuanza mwezi
Machi mwaka 2011.
Uvamizi huo wa jeshi katika mji wa Qusayr ulianza jana huku wapinzani
wa Assad wakionya kuwa mashambulio ya kinyama katika mji huo huenda
ukadidimiza juhudi za Marekani na Urusi za kuandaa mkutano wa amani
unaonuia kumaliza vita hivyo vilivyosababisha vifo vya maelfu ya
wasyria.
Jumuiya ya nchi za kiarabu imeitisha mkutano wa dharura siku ya Alhamisi
wiki hii kabla ya mkutano huo wa amani huku baraza la kitaifa la
upinzani Syria likitaka jumuiya hiyo kukutana na kumaliza kile
ilichokiita mauaji ya halaiki mjini Qusayr.
Huku hayo yakijiri,eneo la Golan linalokaliwa na Israel limelengwa kwa
risasi kutoka Syria usiku wa kuamkia leo lakini hakuna majeraha au
uharibifu ulioripotiwa. Kulingana na msemaji wa kijeshi wa Israel
ufyatuaji huo ulikuwa wa kutumia silaha ndogo na unaaminika haukulenga
milima hiyo kimakusudi.
No comments:
Post a Comment