UBORA wa Taifa
lolote lile hutegemea ubora wa mawazo ya watu wanaounda Taifa hilo pamoja na
nidhamu ya watu wao.
Kwa kuwa mtu
ni mawazo anayofikiri na jamii pia huundwa na mawazo basi kama jamii yetu sio
bora tuangalie upya mawazo yetu sote si kwa kumrushia mpira fulani maana
tunavyofikiri na kuishi ndivyo kizazi chetu pia kitaiga hivyo.
Tujenge familia
zetu na jamii yetu katika fikra sahihi. Baadae yetu itategemea ubora wa fikra
zetu na maamuzi yetu tutakayofanya kwa faida ya kesho.Taifa hili litafika mbali
ikiwa tu tutabadili mwelekeo wa mawazo yetu.
Kuna misingi
miwili kama si mitatu ya baadhi ya viongozi wa CCM itawatoa katika Chama Cha
Mapinduzi.
Misingi hiyo
ni pamoja na CCM ni chama cha kutetea wanyonge lakini siku ikiacha kutetea
wanyonge, wengi wataondoka kwenye chama hicho madhubuti ambacho msingi wa kila
mtu kuwa na haki ndani ya nchi hii kinautetea.
Umoja na
mshikamano aliouacha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.Siku chama
hicho kikiacha kusimamia msingi huo wengi pia watajiengua na chama.
Misingi hiyo
ikisimamiwa vizuri, hakuna mtu atakayekichukia Chama Cha Mapinduzi.
Kwasasa kuna
tatizo ndani ya chama hicho ambalo ama kutofanya maamuzi kwa muda muafaka ama
kufanya maamuzi ambayo siyo sahihi.
Ama
kutochukua hatua katika matatizo yanayowakabili wananchi kwa wakati muafaka,
jambo ambalo linasababisha kero na chuki kwa chama hiki ambacho ni chama imara.
Haya
nimeyabaini baada ya kuwepo huko mjini Mbeya katika sikukuu ya Mei Mosi 2013, ambayo
mgeni rasmi alikuwa ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Nilipokuwa
huko mjini nilijifunza mengi ikiwemo kujua lugha za wanyama ambazo huko mjini
zinathamani kubwa sana kuliko huku kwetu nyikani.
Niliposikia
lugha hizo nikajisogeza na hatimaye kuuliza kuwa mbona huku mjini wanaoitwa
wastaarabu wanazungumza lugha za ndege na wanyama?
Kwanza
nikachekwa kisha wakaniambia kuwa lugha hiyo inaitwa Kiingereza.
Baada ya
kuniambia hivyo kisha nami nikawajuza kuwa lugha hiyo kwetu tumezoea kuiita
lugha ya ndege na wanyama maana ndege na wanyama ndiyo wanazungumza.
Walipojaribu
kuwa makini kwangu nikawaambia kuwa huku kwetu Nyikni Ng’ombe utawasikia
wakisema ‘’More more’’, Mbuzi utawasikia wakisema ‘’Men, Men’’ huku vifaranga
vikisema ‘’New new new’’.
Hapo
walicheka sana na kugundua kabisa kuwa mimi kweli nimetoka Nyikani.
Nianze
kumpongeza sana Rais Jakaya Kikwete kwa kufanikiwa kusikia sauti za wasio
sikika pale mjini Mbeya na hatimaye kuondoka na aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la
Mbeya Jumanne Idd.
Lakini wananchi
wanahitaji kuona hatua za kisheria zinachukuliwa kwa muda muafaka dhidi ya
Mkurugenzi huyo na wenzake hata kama amepata adhabu za kinidhamu vinginevyo wote
wenye mamlaka, wataonekana wanahusika na tuhuma zake kupitia kale kamtindo
ka-kulindana.
Rais
Kikwete, nimerejea salama huku nyikani na sasa nipe muda kidogo wa kunisikiliza
na hapa sikufundishi kazi wala jinsi ya kutimiza majukumu katika serikali yako ‘’sikivu’’.
Wiki ilyopita
nilikueleza Rais Kikwete jinsi gani mimi ninavyoziona kura za udini mwaka 2015
hasa katika nafasi yako kutokana na wewe kusema kuwa hujui yanakotokea masuala
haya.
Leo
nikueleze kuwa Tanzania wakristo na waislam hatuna mgogoro wowote bali ni
serikali yako kukwepa majukumu ya kuwashughulikia ipasavyo wahalifu. Parandesi
hii inaumiza eeh! Niwie radhi.
Walioko
magerezani asilimia 99 wote wana dini zao lakini hawakuhukumiwa kama makosa yao
yalikuwa yametokana na dini zao, bali walihukumiwa kama wahalifu wa kawaida kwa
mujibu wa sheria.
Genge hili
linalotumia kivuli cha dini kufanya uhalifu hapa nchini lishughulikiwe kama
kundi la wahalifu na wala hakuna haja ya kusingizia na kutaka kukaa na viongozi
wa dini, tusikwpe majukumu ya kushughulikia wahalifu.
Hao viongozi
wa dini unaotaka kukaa nao kila linapotokea jambo hawaujui huo unaoitwa mgogoro
kwasababu hawajawahi kugombana na hakuna historia ya hicho serikali yako
inachokiita mgogoro wa kidini.
Kwa
kumalizia kuhusu udini nitoe wito kwa wananchi wenzangu kuwa kundi hili la
wahalifu tuungane na serikali kuliteketeza maana ni kundi ambalo linawinda nchi
zilizotulia kama Tanzania na kwa makusudi hawaendi kwenye nchi zenye vita. Hapo
nimemaliza kuhusu udini.
Rais Kikwete,
sikiliza tena sauti yangu kuhusu serikali yako na chama chako yaani Chama Cha
Mapinduzi(CCM).
Niliwahi
kusema siku za nyuma kuwa mwenye duka ni CCM na muuza duka ni watumishi wa
serikali. Sijui kama ulinitegea sikio au ulikuwa na mambo mengi ya
kushughulikia kuliko kusikiliza sauti yangu kutoka hapa nyikani.
Rais
Kikwete, haya siyo mashairi. Ni ujumbe mzito kutoka huku nyikani kwa msaada wa
wanyonge na hata nyie hapo juu wenye uahueni wa maisha.
Ukiisikiliza
kwa makini sauti hii hasa leo, utagundua kinachowatesa huko serikalini na hata
ndani ya chama unachokiongoza kama Mwenyekiti wake wa Taifa.
Wananchi wa
Tanzania na bahati mbaya hata serikali, wote hamna taarifa sahihi ya kila
upande mahitaji yake na hata kilichofanyika. Ndiyo maana mwenye duka anachukiwa
yaani (CCM).
Serikali ina
uhakika zaidi wa kupata taarifa kutoka kwa wananchi, lakini kwasababu mwajili
wa watumishi wa serikali yaani CCM “madhubuti’’ wanawaogopa wauza duka wao,
basi kila mtumishi anafanya ajualo na hakuna anayejali.
Watendaji wa
chama hicho kwasababu wengi wamekikuta chama na wala hawajawahi kukihangaikia
ndiyo maana wengi hawajali kwa kumaanisha.
Kinachofanyika
ndani ya chama ni kupeana majukumu ya kukilinda chama nyakati za uchaguzi hasa
kwa vijana.
Vijana wa
CCM wanaonekana kila kona ya nchi kila siku nyakati za uchaguzi wakinadi sera
na mambo kadha wa kadha hata wasiyoyajua.
Rais Kikwete
ivumilie Sauti hii kutoka hapa nyikani, ni sauti ya unyonge sana ya mtu
asiyeonekana lakini ni sauti yenye matumaini makubwa kwa wenye mamlaka
mkiisikiliza na kuifanyia kazi.
Vijana wa
CCM wanawezeshwa na kupewa ujasiri, lakini baada ya uchaguzi baadhi yao
asilimia 80 wanakuwa hawajui kinachoendelea! Bila shaka unalijua hili lakini
kimaandishi huko kwenye utendaji wanaonekna kana kwamba wanajua kinachoendelea.
Utekelezaji
wa ilani ya uchaguzi, unaishia mikononi mwa wakurugenzi, copy zake ambazo
ukweli wake unakuwa na mashaka pasipo
shaka wanapelekewa wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa hatimaye CCM
husomewa ripoti hizo zenye mashaka makubwa, lakini nani anajali?.
Rais
Kikwete, hayo yote ni matokeo ya kuwa na kundi kubwa la viongozi wasiojali na
hapa natia shaka ubora wa mawazo yao kwa taifa letu ambapo kila taifa bora
hutegemea mawazo bora ya watu wake.
Wananchi
hawapati taarifa sahihi kutoka serikalini na serikali nayo haipati na haina taarifa sahihi ya mahitaji sahihi ya
wananchi wake “unaweza kupinga, ila pinga kwa hoja siyo malalamiko’’.
Rais
Kikwete, najua baadhi ya watendaji wako wananipuuza na hawataki kuisikia sauti
hii kutoka hapa nyikani lakini naamini wewe huwezi kunipuuza hata kidogo maana
mimi ni mshauri wako wa mambo madogo madogo kwako lakini makubwa na muhimu kwa
wananchi wanyonge na serikali yako.
Wananchi
wana mahitaji yao lakini hakuna mtu wala kiongozi wa serikali anayewauliza
matatizo hayo kama wewe unavyofanya kwenye ziara yako kuwa wananchi wakueleze
matatizo yao.
Wabunge
wengi hata bungeni wanajiwakilisha wenyewe na familia zao maana hata wakija
kwenye ziara huku kwenye majimbo yao wanafanya kama mahubiri kisha ikifika saa
kumi na mbili hufunga mikutano na kuondoka.
Rais
Kikwete, unaweza kushangaa ukienda kwenye kijiji chochote hapa nchini na kuanza
kuzungumza na wananchi. Utakachoambiwa na wananchi hasa mahitaji yao hata madiwani na wabunge
hawajui.
Jaribu
kufanya hivyo na nitazidi kukusisitiza kuhusu ziara za kushitukiza katika mikoa
mbalimbali ingawa uliwahi kusema kuwa kumtoa Rais Ikulu si jambo la kitoto.
Tatizo hapa
ninaloliona ni kuahidi mambo mengi kwa wakati mmoja tena wakati wa furaha hali
ambayo utekelezaji wake unakuwa mgumu.
Kinachotakiwa
kufanyika kwa sasa ni kwamba, kwa kuwa mtu ni mawazo anayofikiri na jamii pia
huundwa na mawazo basi kama jamii tufikirie baadae yetu kwa kuanza sasa kuwa na
ubora wa fikra na maamuzi yetu kwa wakati.
Rais Jakaya
Kikwete, kama kila mmoja atatimiza wajibu wake na tutawajibishana kutokana na
mawazo yetu bora kwa nia ya taifa letu bora na wananchi wakapata taarifa sahihi
na serikali nayo ikawa na taarifa sahihi ya mahitaji sahhi ya wananchi, hakika
hakuna wa kuichukia CCM.
No comments:
Post a Comment