Monday, May 13, 2013

YALIYOJIRI KAMBI YA SIMBA SC ZANZIBAR LEO

HAYA NDIYO YALIYOJIRI KAMBI YA SIMBA SC ZANZIBAR LEO KUJIANDAA NA MPAMBANO DHIDI YA YANGA SC JUMAMOSI

Vijana wa kazi wa jeshi la Msimbazi

Na Prince Akbar, Zanziabr. IMEWEKWA MEI 13, 2013 SAA 12: 40 JIONI
KAMBI ya Simba SC visiwani Zanzibar imekumbwa na misukosuko, baada ya Uwanja wa Chuo cha Elimu Chukwani waliotarajia kuutumia kwa mazoezi kuukuta upo katika ukarabati.
Kwa sababu hiyo, Simba SC imehamia kwenye Uwanja wa Mao Dze Tung, ambao timu nyingi za hapa zinaukataa kwa kudai ni mbaya na unasababisha wachezaji kuumia.
Mratibu wa ziara ya Simba visiwani hapa, Abdul Mshangama ameiambia BIN ZUBEIRY leo visiwani hapa kwamba, baada ya kuona hali ya Uwanja wa Chukwani hairidhishi wameona bora mazoezi yahamie Mao.
Alisema asubuhi walifanya mazoezi nusu Uwanja Chukwani na jioni wakahamia Mao.
Alisema timu iko vizuri na kwa ujumla mazoezi yameanza vizuri leo, kuelekea mpambano dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Tumeipokea timu vizuri, wachezaji wapo katika hali nzuri na wamefikia sehemu nzuri, tulivu na ya amani ili kuweka akili zao vizuri kwa ajili ya kuwashikisha adabu Yanga,”alisema Mshangama.
Simba iliwasili Zanzibar jana jioni kuweka kambi maeneo ya Mbweni JKT katika jumba la kifahari la mpenzi mmoja wa klabu hiyo, Abdul Zacharia kujiandaa na mchezo wa kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Yanga SC Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wakati Simba SC waliwasili jana hapa, wapinzani wao, Yanga wamepitiliza hadi kisiwani Pemba tangu Ijumaa ambako wanajifua vikali pia kwa ajili ya mchezo huo.
Mchezo wa Jumamosi japokuwa hautabdilisha chochote katika msimamo wa Ligi Kuu, Yanga ikiwa tayari bingwa na Simba katika nafasi ya tatu, lakini kwa sababu ya uhasimu wa timu hizo, unatarajiwa kuteka hisia za wengi.
Na kwa kuwa siku hiyo ndiyo Yanga SC watakabidhiwa Kombe lao ubingwa wa Ligi Kuu, Simba SC wamepania kuwafanya mahasimu wao wakabidhiwe ‘mwali’ kinyonge kwa kuwafunga Jumamosi.

No comments:

Post a Comment