Na Edwin Moshi
Kutokana na kusuasua kwa huduma ya chakula kutolewa katika
shule za msingi na sekondari wilayani Makete, kuanzia sasa suala hilo litakuwa
la lazima na si hiari tena kama ilivyozoeleka miongoni mwa wazazi
Akizungumza na ripota wetu, Mkuu wa wilaya ya makete Bi.
Josephine Matiro(PICHANI) ameagiza kuwa kuanzia sasa suala la wanafunzi kupata chakula
shuleni kwao ni lazima hivyo wazazi na walezi wanatakiwa kuunga mkono agizo
hilo kwa manufaa ya wanafunzi hao na taaluma kwa ujumla katika wilaya yake
Amesema wanafunzi kushinda mashuleni bila kula kunasababisha
wao kuona kama wanateswa, na wengi wao wanashindwa kusoma vizuri kutokana na
njaa na matokeo yake wanajikuta wakifeli siku hadi siku
“Tujiulize tu, kila mtu anajua njaa inavyouma, na wazazi/walezi
wa makete hebu tubadilike na tuendane na wakati, kwa karne hii mwanafunzi
kushinda na njaa shuleni hataweza kusoma na kufaulu, ifike wakati sasa
tuchangie ili kila mwanafunzi wa shule yoyote wilayani hapa apate chakula
shuleni” alisema
Ameagiza kuwa suala hilo linatakiwa litekelezwe kwa shule
zote kuanzia muhula wa Julai mwaka huu, na ameahidi kulifuatilia suala hilo
kuona kama linatekelezeka
Kufuatia agizo hilo mwandishi wetu alimfuata afisa elimu
msingi wilaya ya Makete Bw. Antony Mpiluka kumuuliza kuhusu agizo hilo la mkuu
wa wilaya na kusema ofisi yake imelipokea na italifanyia kazi huku akiomba
ushirikiano kwa wazazi kuhakikisha wanachangia ili watoto wawe wanakula shuleni
No comments:
Post a Comment