Wenye simu, mitandao ya kijamii kikaangoni
SERIKALI imesema itachukua hatua kali za kisheria kwa atakayebainika
kutumia vibaya simu za mikononi, na mitandao ya kijamii kuleta uchochezi
au kwenda kinyume cha maadili ya nchi.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa
aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki Dar es Salaam kuwa
lengo la kufanya hivyo ni kukomesha vitendo hivyo kwani ni hatari kwa
nchi. ”Hatua hizo zitachukuliwa dhidi ya kampuni au mtu yoyote
atakayetoa kashafa na kuitukana Serikali, viongozi wa Serikali, dini,
siasa na watu binafsi,” alisema na kuongeza kuwa vitendo hivyo vinakiuka
sheria za nchi.
Alisema hatua hizo zitawakumba pia watu wote wanaojihusisha na
uoneshaji kwenye mitandao hiyo picha za ngono, unyanyasaji wa watoto na
ukiukaji wa maadili na kutoa taarifa zenye lengo la kuvunja utulivu na
amani.
”Matumizi mabaya ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama),
kama za simu za mikononi, barua pepe, na mitandao ya kijamii yanafanywa
na watu wachache kwa kusambaza taarifa zenye nia ya kuchafua taifa
letu,” alisema.
Alisema pamoja na kwamba teknolojia hiyo katika miaka ya karibuni
imechangia kuleta maendeleo makubwa nchini, baadhi ya watu wanaitumia
kwa mambo yasiyofaa.
Waziri alisema kuwa watu wengine wamekuwa wakiitumia kwa kufanya
wizi, ujambazi, ubakaji, biashara ya dawa za kulevya na ukahaba na
kusambaza siri za watu binafsi bila idhini ya wahusika.
Alisema matumizi yasiyofaa yanafanywa na watu wachache yanaelekea
kuharibu maadili ya Watanzania na yanaweza kuhatarisha utulivu na
usalama wa nchi kwa kutumia Tehama. Prof. Mbarawa alisema pia kuwa
hatua kali zitachukuliwa kwa wakala au kampuni ya simu yoyote itakayouza
sim kadi kwa mtu yeyote bila ya kuwa na kitambulisho kinachotambulika
kisheria.
Alisema pia ni kosa la jinai kutoa taarifa za uwongo wakati wa
usajili wa sim kadi na Serikali imejipanga kuzima sim kadi zote ambazo
hazijasajiliwa kama inavyotakiwa kisheria.
CHANZO;NIPASHE
No comments:
Post a Comment