Hii ni kwa sababu Kenyatta angetaka kujisawiri
kama kiongozi wa kisasa. Kiongozi chipukizi ambaye anaenda na wakati
kwani mshuka ngazi na mpanda ngazi, hawashikani mikono.
Mbali na hayo, ameonyesha kwamba kamwe hana
kinyongo na walioshindana naye katika kinyang’anyiro cha urais Machi 4
na amewanyoshea baadhi yao mkono wa amani akiwataka wajiunge naye katika
ujenzi wa taifa.
Tayari amezungumza na kiongozi wa Muungano wa
Amani, Musalia Mudavadi ambaye alizoa kura 400 elfu katika uchaguzi mkuu
na kuwa nambari tatu baada ya Raila Odinga.
Kenyatta pia amefanya mazungumzo ya faragha na
Eugene Wamalawa wa chama cha New Ford-Kenya akitaka ushirikiano naye.
Kuna fununu kwamba anaweza kumpa cheo uwaziri Wamalwa kwa kuwa yeye ni
mwanadani wake kisiasa na vilevile licha ya kuwa waziri wa Haki na
Masuala ya Kikataba, alimtetea vikali kitaka kesi inayomkabili
(Kenyatta) katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa iliyoko The Hague,
Uholanzi ili irejeshwe nchini isikizwe na mahakama za Kenya.
Wamalwa aliacha kuwania urais dakika za mwisho
mwisho. Hatua hii ilionekana na wachanganuzi wa kisiasa kama dalili ya
‘kumuachia’ Kenyatta kura zake ili akishinda amkumbuke katika Serikali
yake. Hii ni kwa sababu Wamalwa angejiaibisha kama angewania urais.
Hangekusanya kura zozote kwa kuwa hana ufuasi mwingi kwa hivyo ilikuwa
jambo zuri kwamba aliamua kutowania urais.
Mwingine ambaye ameafikia mkataba wa kuingia
katika Serikali ya Kenyatta ni Gideon Moi mwanaye, Rais mstaafu Daniel
arap Moi. Chama cha Kanu ambayo kinaongozwa na Gideon hivi majuzi
kiliwekeana mkataba na Kenyatta ili kuipa nguvu Serikali yake na
kuongeza idadi ya wabunge na maseneta.
Jeremiah Kioni ambaye alikuwa mgombea mwenza wa
Musalia Mudavadi pia alikutana na Kenyatta na kukubali kumuunga mkono.
Pilkapilka hizi zote za Kenyatta si za bure na haziko kwenye ombwe tupu.
Kenyatta anafahamu barabara kwamba meli yake ya
uongozi huenda ikakumbwa na misukosuko na dhoruba kali ambazo zaweza
kumtupa kwenye fuo za utawala ama hata kuizamisha.
Hii inatokana na kesi ya uhalifu wa kibinadamu
inayomkabili The Hague. Kesi hii ni donda sugu kwa kiongozi huyu na
imeendelea kumwandama kwa miaka mitatu sasa.
CHANZO ;MWANANCHI
No comments:
Post a Comment