Tuesday, April 23, 2013

HAKUNA TUME YA AJIRA YA POLISI

SERIKALI imesema hakuna tume ya pamoja ya ajira kwa ajili ya askari wa Jeshi la Polisi nchini isipokuwa kuna Tume ya Utumishi wa Polisi na Magereza.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereila Ame Silima alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Fuoni, Said Mussa Zubeir (CCM) aliyetaka kujua kama serikali itakuwa na Tume ya Ajira na Mafao kwa ajili ya askari polisi na magereza.

Mbunge huyo pia alihoji kama tume hiyo ipo, imeweka utaratibu gani wa kulipa askari hao pensheni na motisha pale wanapomaliza kazi zao ikiwemo baadhi ya askari kulipwa sh 785,000 wakati wametumikia nchi kwa muda mrefu.

Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema tume iliyopo ndiyo inayofanya kazi ya kumshauri rais kuhusu uteuzi wa maofisa wa ngazi ya juu na kuwapandisha au kuwashusha vyeo inapothibitika.

“Askari magereza hulipwa pensheni kwa mujibu wa kifungu namba 8 na 9 cha sheria ya mafao ya hitimisho la ajira kwa watumishi wa umma sura ya 371,” alisema Silima.

Kuhusu askari kulipwa sh 785,000 alisema malipo hayo inategemea yalitolewa wakati gani na askari alikuwa akilipwa kiasi gani.

No comments:

Post a Comment