BENDI ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’ inatarajiwa kulindima
kwenye ukumbi wa Aventure mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, kesho kabla
ya kuvamia Triple A jijini Arusha Ijumaa.
Kikosi cha Ngwasuma kinatarajiwa kusheheni nyota wake wote wakiwamo,
‘Prezdaa’ Nyoshi El Saadat ‘Sauti ya Simba’, Patcho Mwamba, Pablo Masai
na Rais wa madansa, Queen Suzzy’.
Shoo hizo za mwisho wa wiki ni sehemu ya kuwapa burudani wapenzi na
mashabiki wao wa Arusha na Moshi, huku wakiwa na lengo la kuonesha
makali yao katika tasnia ya muziki wa dansi nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala
wa Ngwasuma, Kelvin Mkinga, alisema kuwa wanaamini shoo hizo zitawapatia
burudani za aina yake mashabiki wao.
Alisema wanamuziki wao wako kwenye kiwango cha juu kwa ajili ya kutoa
burudani kamili, huku wakiamini kuwa nyimbo zao zitakuwa sehemu moja ya
kuwapa ladha halisi ya Ngwasuma.
“Bendi ni imara na mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa inaendelea
kuwa juu katika tasnia ya muziki wa dansi nchini, kwa kuwatumia vyema
waimbaji wenye vipaji vya aina yake,” alisema.
Aliwaomba mashabiki wa burudani kujitokeza kwa wingi katika shoo hizo,
ambazo ni siku mbili zenye joto la msisimko kwa wadau na wapenzi wa
muziki wa dansi wa FM Academia.
No comments:
Post a Comment