NA IBLAHIM YASIN KWELA
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida iliyowashangaza wengi mganga wa
kienyeji, Edward Mwakalebela (86), anadaiwa kumbaka mtoto wa miaka 6.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Sioni Ijuni, aliiambia Tanzania Daima
Jumatano kuwa mganga huyo mkazi wa kijiji cha Ndwanga, kata ya
Katumbasongwe, wilayani Kyela, mkoani Mbeya, alitenda kosa hilo Aprili
20 mwaka huu majira ya saa 8 usiku.
Alisema aligundua tukio hilo baada ya mtoto wake kulalamika kusikia
maumivu ya tumbo naye kumpa huduma ya kwanza kwa kumkanda na maji ya
moto lakini baadaye aliona damu zikimtoka sehemu za siri.
Alisema alipomhoji zaidi ndipo mtoto huyo alipomtaja babu huyo ambaye
ni jirani yake kuwa alimwingilia kimwili kwa kumfanyia kitendo hicho cha
kinyama.
Kutokana na hali hiyo mama huyo alisema aliamua kupeleka taarifa hiyo
kwa mwenyekiti wa kijiji akiwa na mumewe Kifoji Mwabusila na baada ya
mwenyekiti kuandika maelezo yao aliwaamuru kwenda polisi ili wapatiwe
kibali cha kwenda kutibiwa nao wakafanya hivyo kisha baadaye polisi
walimkamata mtuhumiwa na kumtia mbaroni.
“Tulipokuwa kwa mwenyekiti wa kijiji, babu huyo alikiri kutenda kosa
hilo na aliomba msamaha akidai ni shetani tu alimpitia huku akiomba
mambo hayo yamalizwe kimya kimya bila kwenda polisi jambo ambalo
lilikuwa gumu kwetu,” alisema mama mzazi wa mtoto huyo.
Alieleza kusikitishwa na tukio hilo ikizingatiwa kuwa mzee huyo ni
jirani yake na amekuwa na mazoea ya kumtuma mtoto wake kama mjukuu wake
lakini kumbe alikuwa anatengeneza mazingira ya kumfanyia unyama huo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Dickson Mwakasinga, alikiri kuwepo na
tukio hilo na kueleza kuwa baada ya kupelekewa taarifa ya uwepo wa tukio
hilo alifuata taratibu zote na kumkabidhi mtuhumiwa huyo mikononi mwa
polisi wilaya kwa hatua zaidi za kisheria.
Mganga wa zamu aliyemtibu mtoto huyo, Tabu Mwakalundwa, alikiri
kumpokea mgonjwa huyo na kudai kuwa aliingiliwa na kuharibiwa vibaya na
kwamba wanafanya jitihada za haraka za kumtibu mtoto huyo ili arudi
katika hali yake ya kawaida.
Nao wananchi wa kijiji hicho wamelihusisha tukio hilo na imani za
kishirikina kwa kuwa mzee huyo ni mganga wa kienyeji na kuwa umri
alionao na kitendo alichomfanyia mtoto huyo ni kinyume na maadili ya
Mtanzania.
No comments:
Post a Comment