WANANCHI wa Mkoa wa Ruvuma wametakiwa kulinda na kutunza
barabara zote za mijini na vijini kwa kutong’oa au kuiba alama,
kutoharibu makaravati au vyuma ili kuzifanya zidumu.
Rai hiyo ilitolewa mjini Songea jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said
Mwambungu, alipofungua kikao cha Bodi ya Barabara ya mkoa huo.
Aliwasihi wananchi kutambua umuhimu wa kutunza barabara, kwani zina mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya taifa.
Aidha, amewakemea na kuwaonya wananchi wenye tabia ya kuharibu
miundombinu ya barabara kwa kutupa taka kwenye mitaro ya maji, hivyo
kusababisha barabara hizo kuwa dampo la kutupia takataka badala ya
kupitisha maji.
“Ni muhimu kwa wananchi wetu wote kuelewa na kuchukua hatua za kutunza
miundombinu ya barabara, ili ziendelee kusaidia shughuli za kiuchumi,”
alisisitiza Mwambungu.
Kuhusu makandarasi wanaojenga barabara chini ya kiwango, alisema
serikali haitasita kumfukuza au kumsimamisha mkandarasi yeyote katika
Mkoa wa Ruvuma.
Katika hatua nyingine, mkuu wa mkoa huyo amewafahamisha wajumbe kuwa
mkoa umepiga hatua kubwa ya mafanikio katika sekta ya barabara kwani
jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 245 zimepandishwa hadhi kuwa
za mkoa kutoka halmashauri.
Alizitaja barabara hizo kuwa ni Mlilayoyo-Hanga (kilomita 15.1)
Mtonyi- Naikesi (kilomita 49); zote hizi zipo Wilaya ya Namtumbo na
nyingine ni barabara ya Unyoni-Tingi-Mkenda (kilomita 110.7) iliyopo
wilaya za Nyasa na Mbinga.
Barabara nyingine iliyopandishwa hadhi kuwa ya mkoa ni ile ya Mindu-Ngapa (kilomita 40) iliyopo Wilaya ya Tunduru.
Alisema kutokana na barabara hizo kupandishwa hadhi kutaufanya Mkoa wa
Ruvuma wenye halmashauri tano kuwa na mtandao wa barabara wenye urefu
wa kilometa 3,550.01 kutoka kilometa 3,765.01 za awali.
No comments:
Post a Comment