Saturday, March 9, 2013

MAADHIMISHO SIKU YA AFYA YA FIGO,ARUSHA



WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, amesema Watanzania wataungana na nchi nyingine dunia katika maadhimisho ya ‘Siku ya Afya ya Figo’ inayotarajiwa kufanyika kuanzia Machi 11 hadi 14 mwaka huu.

 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,  Dk. Mwinyi, alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na Chama cha Taifa cha Afya ya Figo, itaadhimisha  siku hiyo kitaifa katika viwanja vya Hospitali ya AICC, mkoani Arusha.

 Kaulimbiu yake  ya maadhimisho hayo ni ‘Epuka Kuharibu Figo’.
Alisema katika kuadhimisha siku hiyo wataalamu mbalimbali watatoa elimu kuhusu umuhimu wa figo katika kudumisha afya ya jamii.
Alisema siku hiyo kutatolewa huduma ya upimaji figo bila malipo, kwa kila mwananchi atakayefika katika viwanja hivyo.


“Maradhi haya yanawapata watu wengi hasa baadhi ya vijana na watu ambao wamekuwa wakipata magonjwa ya kuambukiza kama vile kuhara, malaria, dengue, homa ya ini, pepopunda na ukimwi,” alisema.

 Mjumbe wa chama hicho, Linda Ezekiel, alisema hadi sasa wagonjwa 1550 walijitokeza hospitalini katika kipindi cha mwaka jana ambapo walichunguzwa na wengine kupatiwa matibabu. 

Hata hivyo, alisema wapo wagonjwa 14 ambao hali zao zinahitaji matibabu zaidi, wanatarajiwa kusafirishwa kwenda India wakati wowote kuanzia sasa.

No comments:

Post a Comment