Saturday, February 16, 2013

UFAFANUZI KUHUSU CHANJO YA UKIMWI HUU HAPA

JOPO la Madaktari wa Chuo wa Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), wametoa ufafanuzi kuhusu majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa Ukimwi, wakisema bado wanaendelea kuifanyia utafiti zaidi.
Kiongozi wa Jopo la Madaktari hao lililofanya utafiti huo, Profesa Muhammad Bakari aliliambia gazeti hili kuwa ingawa majaribio ya chanjo hiyo yaliyofanyika nchini mwaka 2007-2010 na 2008-2012, yameonyesha mafanikio mazuri, lakini majaribio hayo hayajafikia hatua ya kupatikana kwa chanjo kamili.
Alisema majaribio hayo, yamethibitisha kuwa chanjo ya DNA - MVA ilikuwa salama na yenye uwezo wa kuufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi (VVU).
Profesa Bakari ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu Chuo cha MUHAS, alisema baada ya kuanza kufanya utafiti, jopo la madaktari bado liliendelea na utafiti zaidi, ulioanza mwaka 2008 hadi 2012 ili kupata chanjo.
“Hatukuishia hapo, utafiti wa pili (TAMOVAC-01), ulifanyika kati ya mwaka 2008 na mwaka 2012. Utafiti huu ulijumuisha pia nchi jirani ya Msumbiji.

Alisema utafiti wa awali ambao ulijulikana kama HIVIS-03, ulihusisha askari 60 ambao walifuatiliwa kwa karibu wakati wote wa utafiti ili kuhakiki usalama wa chanjo na uwezo wa chanjo kute ngeneza vichocheo vya kinga dhidi ya VVU.
Juhudi za kukabiliana na VVU zimekuwa zikifanywa na wanasayansi mbalimbali duniani lengo likiwa ni kupata chanjo ama dawa ya kutibu. Kwa sasa waathirika wamekuwa wakitumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV).

No comments:

Post a Comment