WIKI moja baada ya Chadema kufanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Temeke Mwisho jijini Dar es Salaam na kuwashukia Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, CCM jana ilifanya mkutano katika viwanja hivyo, huku ikijibu hoja zilizotolewa na chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Mkutano huo wa Chadema ulifanyika Jumapili
iliyopita, ambapo viongozi wake walitoa tuhuma mbalimbali kueleza jinsi
Spika Makinda na naibu wake walivyotupa hoja za Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika na James Mbatia ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Maji
Profesa Jumanne Maghembe alisema hoja ya Mnyika kuhusu uhaba wa maji
katika Jiji la Dar es Salaam, ilitupwa kwa kuwa alichokuwa akikizungumza
mbunge huyo, kilikuwa kikifanyiwa kazi na Serikali.
“Mnyika anatakiwa kutosherehekea mimba wakati
mwenye mtoto ni CCM, Serikali ya CCM ndiyo imeweka miradi iliyopo katika
Jimbo la Ubungo na inaiendeleza,” alisema Maghembe.
Alifafanua kwamba Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini
utakamilika kujengwa mwishoni mwa mwezi huu na utazinduliwa na Rais
Jakaya Kikwete.
“Serikali imejianda kuhakikisha kwamba Mkoa wa Dar
es Salaam unakuwa na maji ya kutosha katika mpango wake wa muda mfupi
na mrefu. Katika mpango wa muda mfupi mpaka kufikia Aprili 2014, maji
yatakuwa ya kutosha katika jiji hili,” alisema Maghembe.
Alisema kuwa hivi sasa Serikali ipo katika mpango
wa kutandaza mabomba ya maji kutoka Ruvu Juu kwenda Dar es Salaam
kupitia Bagamoyo, ambapo utaenda sambamba na uchimbaji wa visima 84.
Katika mkutano huo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Kilimo, Mifugo na Maji, Neema Himid alisema kuwa hoja iliyowasilishwa na
Mnyika bungeni ilikuwa ni; ‘Copy and Paste’, (ya kamati hiyo).
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa
CCM akiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, baadhi ya wabunge
wa Mkoa wa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment