Saturday, February 16, 2013

ALIYEMUUA MPENZI WAKE AFIKISHWA

MKIMBIAJI mlemavu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius (26) jana alimwaga chozi alipofikishwa mahakamani kusomewa shtaka la mauaji ya mpenzi wake wa kike, Reeva Steenkamp (30), pichani chini.
Mauaji hayo yameshitua watu wengi nchini Afrika Kusini hasa kwa vile mpaka mpaka sasa chanzo cha mauaji hakijajulikana.
Nyota huyo wa Paralympiki, alisomewa shtaka la kumpiga risasi na kusababisha kifo cha mpenzi wake huyo ambaye ni mwanamitindo.
Alisomewa shtaka lake asubuhi na mapema kwenye mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Pretoria ambapo alionekana kuwa na huzuni kubwa.
Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa kosa hilo lina adhabu kali ya kifungo cha maisha.
Mbele ya ukumbi wa mahakama, Pistorius alikosa raha na ilikuwa kazi kubwa kwa baba yake, dada na kaka kumtia moyo.
Mwili wa Steenkamp ulikuwa na majeraha manne ya risasi alizopigwa nyumbani kwa Pistorius.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa, muuaji alimlenga mwanadada huyo kupitia mlango wa bafu la nyumba ya mkimbiaji huyo.
Pistorius alizaliwa bila miguu na amekuwa akishinda kwa kutumia miguu ya bandia.
Umaarufu wake ulijulikana zaidi baada ya kukimbia na watu wenye viungo kamili na kufanya vizuri.
Majirani wa mwanariadha huyo walisema kuwa, walisikia mlio mmoja wa risasi kisha kikafuata kimya cha dakika 10, ndipo iliposikika milio mingine mitatu.
Silaha iliyotumika kwa mauaji hayo inashikiliwa na polisi kama kielelezo cha ushahidi.

No comments:

Post a Comment