WAKATI watanzania wengi hawajasahau machungu ya kulizwa na
kampuni ya kupanda na kuvuna mbegu ya DECI, kumeibuka taasisi mpya ya
fedha inayojitapa kutoa mikopo kwa njia ya mtandao, huku ikitumia vibaya
majina ya Rais Jakaya Kikwete na Barack Obama wa Marekani.
Mbali ya taasisi hiyo ya Tanzania Loans Society kutumia majina ya
marais hao, imewahusisha pia Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Ridhiwani
Kikwete, ambapo inahofiwa kutapeli mamilioni ya walalahoi.
Taarifa za taasisi hiyo zinaonesha kuwa ilianza shughuli zake mwaka
2012, na kupata ufadhili wa fedha kutoka kwa Rais Obama, ambapo
inasimamiwa na Rais Kikwete, Waziri Mkuu Pinda na mratibu mkuu ni
Ridhiwani.
Watendaji wengine ni Michael John ambaye namba yake ya simu ya mkononi ndiyo inayotumika kutuma pesa za usajili.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa taasisi hiyo,
imekuwa ikijitangaza kutoa huduma ya mikopo na mawasiliano ya jinsi ya
kupata mikopo hiyo, hufanyika kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha wateja
wa mikoani kupata mikopo hiyo kirahisi bila usumbufu wa kuja makao
makuu yao jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi walioomba kupata mikopo hiyo, waliliambia gazeti
hili kuwa, fomu za mikopo ya taasisi hiyo hutolewa kwa sh 15,000 ambazo
nazo hulipiwa kwa njia ya mtandao.
Mmoja wa wateja wa taasisi hiyo aliyedai kutapeliwa, Maywood Maganga
alisema alionja machungu baada ya kuingia kwenye tovuti yake na
kukutana na maelekezo ya kumtaka ajaze fomu na taarifa zake binafsi
na kisha kutakiwa kutuma sh 15,000 kwenda kwenye namba 0656 73 64 16,
iliyosajiliwa kwa jina la Michael John.
Maganga alisema kuwa alifanya hivyo, na kusubiri majibu.
Kwa mujibu wa mkopo huo wenye masharti nafuu, tena usio na riba, mteja
hutakiwa kurejesha na kuanza kukatwa baada ya miezi miwili tangu siku
ya kupokea pesa hizo za mkopo.
“Maelezo ya mkopo huo yanaonesha kuwa una masharti nafuu sana na
marejesho yake ni sh 60,000 kila mwezi bila kujali kiasi ambacho mteja
amekopa.
“Maelezo ya fomu niliyojaza yalinionesha kwamba nitapata sh 300,000
kama zawadi kwa kukubali kukopa na baada ya dakika 30, ningeingiziwa
kiasi cha fedha za mkopo nilizoomba,” alisema.
Kwa mujibu wa Maganga, fomu alizozikuta kwenye tovuti ya taasisi hiyo,
zilionesha mahala ofisi ilipo, lakini alipofuatilia na kuuliza,
alibaini kuwa taasisi hiyo haina ofisi katika jengo la serikali la
Utumishi wa Umma.
“Mwanzoni sikuwaza kama taasisi hii itakuwa ya kitapeli, lakini baada
ya siku mbili ya kutokutumiwa pesa hiyo ndipo nilipogundua kwamba
nimetapeliwa,” aliksema.
Maganga aliziomba mamlaka husika kuingilia kati kwa kudhibiti utapeli
huo, kwani Watanzania wengi wameshalizwa kupitia taasisi hiyo inayotumia
majina ya watu maarufu kutapeli.
Aidha, maelezo ya tovuti hiyo yanaeleza zaidi kuwa kwa kutambua ugumu
wa maisha uliopo kwa Watanzania na kukua kwa teknolojia kama nchi
zingine zifanyavyo, taasisi hiyo inatoa mikopo kwa njia hiyo ya
mtandaao ili kuepuka usumbufu wa kuwafikia watu walioko mikoani ili nao
wanufaike.
Mbali ya hayo, pia taarifa ya maelezo ya taasisi hiyo hiyo ilieleza
kuwa kiwango cha chini cha kupata mkopo ni sh 100,000 na ofisi zake
zipo katika jengo la utumishi wa umma, ghorofa ya tano chumba namba 30.
Ridhiwani hakuweza kupatikana kuzungumzia taasisi hiyo, lakini katika
taarifa aliyoituma hivi karibuni kwenye ukurasa wake wa facebook,
alikanusha yeye na viongozi wa serikali akiwemo Rais Kikwete kuhusika na
taasisi hiyo.
“Maisha ni kuhangaika na kwamba inataka mtu anayefahamu njia sahihi
kuweza kujua kuwa nikitumia njia hii hali itakuwa sawa na pengine mambo
yangu yatanyooka.
“Hii inaweza kuwa ndiyo maana halisi ya kuhangaika ufanikiwe, lakini
tafsiri hii haiwezi kuwa kutumia njia za kudhulumu, kukaba, kuiba au
kufanya utapeli ili ufanikishe malengo yako mabaya dhidi ya mtu au
kikundi fulani cha watu," aliandika Ridhiwani kwenye ukurasa wake wa
facebook.
Kwa mujibu wa Ridhiwani, hivi karibuni alipokea ujumbe mfupi wa
maandishi kupitia simu yake ya mkononi na barua pepe, ikihoji kuhusika
kwake na kampuni hiyo.
Alisema mradi huo unadaiwa kuanzia katika mikono ya Rais Obama kuja
Tanzania kupitia Kikwete na sasa yeye akishirikiana na Waziri Mkuu
Pinda wanauendesha.
“Jambo hili si la ukweli hata kidogo, na naomba kutumia nafasi hii
kulikanusha kabisa mbele ya umma wa Watanzania na wale wote ambao kwa
namna moja au nyingine wanafuatilia,” ilisema taarifa hiyo ya Ridhiwani.
Vilevile taarifa ya Ridhiwani ilitahadharisha umma wa Watanzania kuwa
makini na mambo ya mitandao ambayo hutumia jina lake kwa utapeli kwa
lengo la kumchafua, lakini yeye na viongozi wengine hawahusiki na
Tanzania Loans Society.
Viongozi wa taasisi hiyo hawakuweza kupatikana kwa njia yoyote ile
kwani simu zao hazipokelewi na hata katika ofisi wanazodai kuwapo,
hawaonekani.
No comments:
Post a Comment