Nyumba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
imeponea chupuchupu kuchomwa moto na wananchi waliokuwa na hasira
kutokana na kukatika maji wiki mbili mfululizo.
Aidha, mkoani Dar es Salaam jana kulikuwa na maandamano ya wanawake na watoto wa eneo la Kimara ambao ilielezwa walikuwa wakitaka kwenda nyumbani kwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kuelezwa hatma ya upatikanaji maji ili waondokane na gharama kubwa kuyanunua.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alisema wiki iliyopita kwamba umati wa watu uliingia kwa nguvu nyumbani kwake na kumimina maji yote aliyokuwa amehifadhi.
“Wiki iliyopita nusura nyumba yangu ichomwe moto… kwani maji yalikatika hapa kwa wiki mbili na wananchi kuamua kuvamia kwangu na kujimiminia maji yote niliyokuwa nimehifadhi kwa ajili ya matumizi yangu,” alisema.
Alitoa taarifa hiyo kwa Waziri wa Maji, Profesa Maghembe aliyekuwa mkoani humo kwa ajili ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji wa awamu ya pili wa Chalinze.
Aliendelea: “Mheshimiwa Waziri mimi pale nyumbani nina walinzi wawili, wananchi waliamua kutumia nguvu na kujimiminia maji…sasa fikiria kama wasingekuta maji yaliyohifadhiwa nyumbani kwangu naamini kabisa nyumba yangu wangeiteketeza kwa moto.”
Akizungumza akiwa Vigwaza, Mwantumu alisema kuchelewa kukamilika kwa mradi huo kumezua mgogoro mkoani mwake.
Alisema wananchi walichukua uamuzi wa kuvamia nyumba yake wakiamini kuwa hali hiyo ingesababisha Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasco) kufungua maji. CHANZO ;:http://eddymoblaze.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment