WAKATI mjadala wa matokeo mabaya ya kidato cha nne ukiendelea kulitikisa taifa, kashfa mpya ya matokeo hayo imeibuliwa.
Kashfa hiyo mpya imeibuliwa na Mkurugenzi wa Shule ya Green Acres,
Julian Bujugo, kwamba matokeo ya baadhi ya shule nchini ikiwamo yake
yamechakachuliwa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Bujugo alisema kuwa baadhi ya
wanafunzi kwenye shule yake hawakufanya mitihani ya kidato cha nne,
lakini matokeo yanaonesha wamefaulu kwa kupata alama za juu.
Alitaja mfano wa mwanafunzi, Humphrey Sanga, mwenye namba 01197/148,
ambaye hakufanya mitihani hiyo lakini matokeo yanaonesha amefaulu kwa
kupata alama nzuri.
“Huyu mwanafunzi tulimsimamisha na hakufanya mitihani, lakini matokeo
yake yanaonekana amepata hivi; Civics D, Historia D, Jiografia C,
Kiswahili D, English C, Physics D, Chemistry C, Biology C, Basic
Mathematics D, ambapo amepata daraja la tatu pointi 24,” alisema Bujugo.
Alimtaja mwanafunzi mwingine, Martin Rushaigwa, namba 01197/0173, ambaye alifanya masomo ya ‘Arts’.
Alisema matokeo ya mwanafunzi huyo yanaonesha kuwa ameongezewa alama
za masomo ya biashara ya Bookeeping na Commerce, ambayo hakuyafanya
kabisa.
Alimtaja mwanafunzi mwingine aliyefanya mtihani huo lakini matokeo
yake yanaonesha amewekewa ‘absent’ na mwanafunzi mwingine, Mbazi Volta,
hakufanya mitihani lakini amepewa alama za ufaulu.
“Matokeo hayo yananipa wasiwasi kwamba yanaweza kuwa yamechakachuliwa,” alisema Bujugo.
Mkurugenzi huyo anaiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kurudia
kusahihisha mitihani hiyo ili kuondoa ukungu ulioligubika taifa kwa sasa
kuhusu matokeo ya kidato cha nne.
“Naomba usahihishaji urudiwe, maana huu ni ubabaishaji mkubwa…matokeo
hayo yamewaathiri watoto kisaikolojia na sijui watakwenda wapi?,”
alihoji.
Alisisitiza kuwa usahihishaji urudiwe kwani katika shule hiyo
wanafunzi wenye uwezo mkubwa tangu walipoanza kidato cha kwanza ndio
waliofanya vibaya wakati waliokuwa wakifanya vibaya, wameibuka na alama
za juu.
Mkurugenzi huyo alisema wazazi wa watoto hao wanatarajiwa kukutana
mwishoni mwa wiki hii kujadiliana kuhusu matokeo hayo na hatua za
kuchukua.
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Msemaji wa Baraza la Taifa la Mitihani
(NECTA), John Nchimbi, alisema si kweli kuwa matokeo hayo
yamechakachuliwa bali ni matokeo halisi ya shule hiyo.
Alisema iwapo mkurugenzi wa shule hiyo ana shaka na matokeo hayo,
alitakiwa kufika katika ofisi za baraza hilo ili apatiwe taarifa sahihi
kabla ya kutoa taarifa katika vyombo vya habari.
“Mi nimeangalia hayo majina, naona yapo sawa na hata huyo mwanafunzi
ambaye anasemekana hakufanya mitihani na akapewa alama…napenda kusema
kuwa alama alizopewa si zake na hata katika orodha yetu anaonekana kuwa
hakufanya mitihani,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa na
wenzake, wamekuwa bubu kueleza endapo wako tayari kujiuzulu au la.
Tanzania Daima ilifika wizarani hapo jana kutaka kuonana na Waziri
Kawambwa ili atoe msimamo wake, mwandishi alijibiwa kuwa waziri huyo
alikuwa kikaoni na asingeweza kutoka.
Hata waziri alipopigiwa simu pamoja na kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakupokea wala kujibu ujumbe huo.
Kwa upande wake, katibu mkuu wa wizara hiyo naye hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa alikuwa kikaoni.
Naye Naibu Waziri, Philipo Mulugo, alipotafutwa kupitia simu yake ya
mkononi kueleza msimamo wake, simu yake iliita bila kupokewa na hata
hakuwa tayari kujibu meseji ya ujumbe mfupi.
No comments:
Post a Comment