Wednesday, February 20, 2013

HALI YACHAFUKA MAZISHI YA PADRE ZANZIBAR

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, amechafua hali ya hewa wakati wa mazishi ya Padri Evaristus Mushi, aliyeuawa kwa kupigwa risasi Visiwani Zanzibar.
Hali hiyo iliyosababisha waziri huyo azomewe, ilitokea jana kwenye mazishi ya padri huyo, yaliyofanyika katika makaburi ya watawa, yaliyopo eneo la Kitope, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Mbele ya Rais wa SMZ, Ali Mohamed Shein, Waziri huyo aliwachefua maelfu ya Wakristo waliofurika kwenye mazishi hayo wakati akitoa salamu za pole kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Katika salamu hizo, waziri huyo alianza vizuri kwa kutoa pole na kwamba serikali imeguswa na kifo hicho na maumivu waliyonayo waumini ndiyo iliyonayo pia serikali.
Lakini wakati akiendelea kutoa salamu hizo, alichafua hali ya hewa kwa kusema kifo cha Padri Mushi kimetokana na mapenzi ya Mwenyezi Mungu.
“Ndugu zangu poleni kwa msiba huu, serikali imeguswa sana na kifo hicho kama ndugu na waumini mlivyoguswa. Hata hivyo hii ni mipango na mapenzi ya Mwenyezi Mungu…”
Kauli hiyo ilisababisha umati wa watu waliofurika katika makaburi hayo kupaza sauti kwa kuzomea na kuikejeli Serikali ya SMZ kwamba kifo hicho hakikutokana na mapenzi ya Mungu.
Katika zogo hilo, wapo waliopaza sauti kwa kusema kifo hicho hakikutokana na mapenzi ya Mungu, kwani hakufa kwa ajali ya maji, ajali ya gari wala kugongwa na gari.
“Hatutaki kusikia hilo, Padri Mushi hakufa kwa mapenzi ya Mungu. Hatutaki kusikia… huo…” zilisikika sauti za baadhi ya watu waliohudhuria mazishi hayo.
Wakati zogo hilo linaendelea, Waziri Aboud alishindwa kuendelea kutoa salamu hizo, hali iliyosababisha Askofu wa Jimbo la Zanzibar, Dk. Augustino Shao kuingilia kati.
Shao aliungana na waumini kwa kusema kifo cha Padri Mushi hakikutokana na mapenzi ya Mungu bali kimetokana na magaidi waliokatiza uhai wake.
Kauli hiyo iliibua kelele za shangwe kutoka kwa waumini hao ambao waliendeleza kelele za kumzomea Waziri Aboud.
Askofu Shao alisema wakati huu si wa kukumbatia maovu na kusisitiza kifo cha Padri Mushi hakikutokana na mapenzi ya Mungu, bali kimefanywa na watu wakatili waliokatiza maisha yake.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa wakati akitoa salamu za chama chake, alisema kuwa taifa liko katika hatari ya kusambaratika kwani kuna viashiria vya wazi vinavyoonesha kuwa tuko katika wakati mgumu.
Alivitaja viashiria hivyo kuwa ni pamoja na kuuawa kwa kupigwa risasi Padri Mushi, kupigwa risasi kwa Padri Ambrose Mkenda, kuuawa kwa mchungaji Geita katika mzozo wa kuchinja, kuuawa kwa mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi na matukio mengine.
Dk. Slaa alitofautiana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete kutaka kuleta wachunguzi kutoka nje, akisema hatua hiyo ni sawa na kushughulikia tawi badala ya kukata shina na mizizi.
Mbali ya matukio hayo, ibada ya kumuaga padri Mushi ilianza saa mbili asubuhi na kufanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, katika eneo la Minara Miwili mjini hapa.
Pengo aongoza misa
Misa hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na kufuatiwa na maandamano yaliyokuwa na ulinzi mkali kuelekea katika makaburi ya Kitope.
Maaskofu wengine waliohudhuria ni Balozi wa Baba Mtakatifu, Askofu Mkuu Frachesco Padilah, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Tarcius Ngalalekumtwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora, Paulo Ruzoka, ambaye pia ni msimamizi wa kitume wa Jimbo la Kigoma na Askofu wa Mahenge, Agapitus Ndorobo.
Wengine ni Askofu wa Tanga, Anthony Banzi, Askofu Renatus Mkwande wa Bunda, Askofu Gervas Nyaisonga wa Dodoma, Askofu Damian Dallu wa Geita na mwenyeji wao, Askofu Agustino Shao wa Zanzibar, akiwamo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustine, Dk. Charles Kitima.
Maaskofu wengine waliohudhuria ni pamoja na Askofu Mstaafu wa Anglikana Zanzibar John Ramadhan, Askofu Mkuu wa KKKT Tanzania, Dk. Alex Malasusa akiwakilishwa na wachungaji, Charles Mgena na George Fupe.
Viongozi wa serikali waliongozwa na Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein, Makamu wa Kwanza, Maalim Seif na mawaziri Mwinyi Makame, Mohammed Aboud na Said Mbaruku.
CHADEMA iliwakilishwa na Dk. Wilbrod Slaa na James Mbatia (NCCR-Mageuzi).
Hotuba ya Baba Mtakatifu yaliza wengi
Hotuba ya Baba Mtakatifu, Benedict wa 16 iliyosomwa na Balozi wake, Padilah, iliwaliza wengi.
Baba Mtakatifu pamoja na kueleza kushitushwa kwake na mauaji ya Padri Mushi, alisema hata kama watumishi wake watashambuliwa, watatakiwa kujibu kwa upendo na kufanya kazi za utume kwa nguvu kwa kuwapenda hata maadui.
Alisema kifo cha Padri Mushi kisiwakatishe tamaa ya kufanya utume wao.
“Watu fulani wamemkatisha maisha yake. Hatuelewi kwa nini mtu mwema ananyimwa nafasi ya kutimiza kazi yake. Naamini Yesu atatusaidia kutimiza, maana hili ni jaribio la imani yetu,” imesema sehemu ya hotuba hiyo.
Padri aliyejeruhiwa kwa risasi aibuka
Padri Ambrose Mkenda, aliyepigwa risasi na kujeruhiwa vibaya amepata nafuu na kushiriki ibada ya misa ya kumuombea Padri Mushi, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jana jioni.
Kuhudhuria kwa Padri Mkenda katika ibada hiyo maalumu kulitangazwa na Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa, ambaye alikuwa akiiongoza.
Hatua ya kumtambulisha Padri Mkenda kuhudhuria ibada hiyo naye akasimama, ilishangiliwa na waumini wa kanisa hilo waliohudhuria misa hiyo kwa kupiga makofi na vigelegele.

No comments:

Post a Comment