MHITIMU wa kidato cha nne jijini Dar es Salaam, Barnaba Venant
(18), amejinyonga baada ya kutoridhishwa na matokeo ya mtihani wake,
yaliyotangazwa juzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiyondo, alisema tukio
hilo la kusikitisha lilitokea juzi, majira ya saa nne asubuhi katika
eneo la Nzasa, Mbagala ambapo kijana huyo alijinyonga kwa kutumia kamba
ya manila, aliyotundika kwenye dari ndani ya stoo ya nyumba yao.
Kiyondo alisema Venant alimaliza kidato cha nne mwaka jana katika
Shule ya Sekondari Debrabant, Mbagala, huku akielezea kuwa sababu ya
kujinyonga kwake ni kutoridhishwa na matokeo ya mtihani wake ambapo
alipata daraja la nne la pointi 27, kinyume na matarajio yake.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke wakati upelelezi wa tukio hilo unaendelea.
Matokeo kidato cha nne mwaka huu, yamekuwa gumzo kutokana na kiwango cha ufaulu kushuka kwa kasi ya kutisha.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, jumla ya watahiniwa 240,903, sawa na
asilimia 60 ya watahiniwa wote, wamepata ziro ambapo kati yao wasichana
ni 120,239 na wavulana 120,664.
Wakati huohuo, watu wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti,
likiwemo la mkazi wa Kisensera Bunju B, Miraji Sewia (30) kukanyagwa na
gari baada ya kulidandia na kudondoka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema kuwa
ajali hiyo ilitokea juzi katika barabara ya Bunju eneo la Kisensera
ambapo gari aina ya Fuso yenye namba za usajili T 614 AQX iliyokuwa
ikiendeshwa na Freddy Ndenasi (45) ilimkanyaga Sewia na kufariki
papohapo.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kenyela alisema mkazi wa Mikocheni
alijefahamika kwa jina moja la Mzee Selemani, amefariki dunia katika
mazingira ya kutatanisha.
Alisema chanzo cha kifo hicho hakijafahamika na mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment