Wednesday, February 27, 2013

LOWASA AICHANA CCM

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amesema kuwa iwapo serikali zote mbili; ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar, zitatekeleza kwa usahihi maelekezo ya mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juu ya suala la ajira, chama hicho kitashinda kiurahisi katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Akizungumza kuhusu uchaguzi wa Kenya, Lowassa alisema amefurahishwa na jinsi Wakenya walivyolichukulia tatizo la ajira kama moja ya ajenda muhimu katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.

Alisisitiza kuwa, kama CCM nayo italichukua tatizo la ajira kwa vijana kama moja ya ajenda yake, kitashinda kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa urais kabisa.

“Moja ya maazimio ya mkutano mkuu wa CCM ni juu ya suala la ajira, na katika kikao cha Halmashauri Kuu hivi karibuni, tulilijadili kwa kina tatizo hili, na kwa kweli kama serikali zetu hizi zitatekeleza maelekezo yake, sina shaka yoyote CCM tutashinda kiurahisi 2015,” alisema.

Lowassa ambaye amekuwa msemaji mkuu wa suala la ajira kwa vijana akiliita kuwa “ni bomu linalosubiri kulipuka”, aliongeza kuwa uamuzi wa vikao hivyo ukitekelezwa vizuri utaifanya CCM iingie kwenye uchaguzi mkuu ikiwa na majibu sahihi yaliyokwishajibiwa juu ya tatizo la ajira kwa vijana.

No comments:

Post a Comment