Saturday, February 9, 2013

HATIMAYE MATUMAINI ATOKA HOSPITALI

 
Na Elizabeth John

MUIGIZAJI wa filamu za kibongo na mchekeshaji, Tumaini Martin ‘Matumaini’ ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam ambako anatarajiwa kurejea tena baada ya kumaliza dozi ya dawa alizopewa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, rafiki wa karibu wa msanii huyo, Robert Kiwewe ‘Kiwewe’ alisema kuwa, Matumaini alilazwa hospitalini hapo kwa siku tatu akiwa anasumbuliwa na miguu, ambako juzi aliruhusiwa kurudi nyumbani.

“Hivi nimetoka nyumbani kwao Yombo kumuangalia, bado hali yake sio nzuri, daktari kampa dawa, kamwambia arudi hospitali baada ya kumaliza kumeza dawa hizo, Watanzania tunatakiwa kumuombea mwenzetu ili arudi katika hali yake ya kawaida,” alisema Kiwewe.

Alisema hali yake sio nzuri, kwani hadi sasa hajui ugonjwa unaomsumbua, taarifa walizozipata mwanzo ni kwamba alianza kusumbuliwa miguu, ikafuata na mikono na sasa maumivu yamesambaa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kiwewe alisema kuwa, kutokana na kushindwa kugundua ugonjwa unaomsumbua, daktari ameamua kumpa dawa za kupunguza maumivu.

Alisema kwa sasa hawana utaratibu mwingine ambao wameweza kuufanya hadi amalize kumeza dawa hizo na kurejea tena hospitali.

Matumaini alikwenda kuishi nchini Msumbiji na kuripotiwa kusumbuliwa na maradhi, lakini alishindwa kutibiwa akiwa huko ambako Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla akishirikiana na baadhi ya wasanii, alichukua jukumu la kutoa nauli ya kumrudisha nchini.

No comments:

Post a Comment