DEREVA maarufu wa pikipiki za abiria ‘bodaboda’ mjini Mpanda,
Selemani (35) amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela kwa kosa la
kuingilia msafara wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati wa ziara yake
mkoani Katavi hivi karibuni.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya
Wilaya ya Mpanda, Chiganga Tengwa, na kuwashitua wakazi wengi wa mjini
Mpanda.
Awali Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Ally Mbwijo aliiambia mahakama kuwa
Selemani, maarufu kwa jina la Baunsa alitenda kosa hilo Desemba 16
mwaka jana majira ya saa 11 jioni katika eneo la benki ya CRDB wakati
Pinda alipokuwa akirejea nyumbani kwake Mtaa wa Makanyagio akitokea
wilayani Mlele.
Alieleza mahakamani hapo kuwa, pamoja na Selemani kusimamishwa na askari
wa usalama barabarani ili aupishe kwanza msafara huo, hakuweza kutii
agizo hilo, jambo ambalo lilikuwa ni hatari.
Aliongeza kuwa, polisi waliamua kumfukuza na kumkamata, lakini
aliwagomea kumpeleka kituo cha polisi kwa kile alichodai hawezi kwenda
hadi atakapofika Kamanda wa Polisi wa Mkoa kwa kile alichokidai askari
wa usalama barabarani wamemuonea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari ambae nae alikuwa
kwenye msafara huo, alifika kwenye eneo hilo na kuamuru mwendesha
pikipiki huyo apelekwe kituo cha polisi, agizo ambalo lilitekelezwa na
mshitakiwa alitii amri.
Makosa mengine yaliyokuwa yakimkabili mshtakiwa huyo ni pamoja na
kuendesha pikipiki akiwa amelewa, kuendesha pikipiki bila leseni na
kukaidi amri halali ya polisi.
Hakimu Tengwa baada ya kusikiliza kesi hiyo alisema mahakama imeridhika
na ushahidi na utetezi na kumtia hatiani, akamhukumu kulipa sh laki tano
ama kwenda jela miezi mitatu, licha ya mshitakiwa kuomba aachiwe huru
akidai askari waliomkamata kwenye eneo hilo walimfananisha.
No comments:
Post a Comment