SAKATA la kuhojiwa kwa Mhariri wa gazeti la Tanzania Daima
Jumamosi, Charles Misango, pamoja na mwandishi, Josephat Isango, kwa
madai ya kuandika habari ya uchochezi limechukua sura mpya, baada ya
Jeshi la Polisi nchini kudai kuwa linamtafuta Mkurugenzi wa Kampuni ya
Free Media Limited, Dk. Lilian Mbowe, kwa ajili ya mahojiano.
Mbali na Dk. Mbowe, polisi imetangaza kumsaka Mhariri Mtendaji wa
Tanzania Daima, Ansbert Ngurumo, pamoja na uongozi wa Kampuni ya
uchapaji ya Printech, iliyochapa gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi
Februari 16.
Misango na Isango walikamatwa juzi asubuhi na kuhojiwa hadi saa moja
jioni kabla ya kuachiwa kwa dhamana kutokana na habari iliyoandikwa na
gazeti hili na kupewa kichwa cha habari; ‘IGP na Wassira watimuliwa
Geita’.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi pamoja na Ikulu walikanusha tuhuma hizo
siku hiyo hiyo, ambapo kufuatia uchunguzi mpya wa habari hiyo, Mhariri
Misango aliwasiliana kwa njia ya simu na msemaji wa jeshi hilo, Advera
Senso, kumjulisha juu ya upungufu huo na siku iliyofuata, Jumapili
Februari 17, gazeti hili lilisahihisha na kuwaomba radhi Waziri
Stephen Wassira na IGP Said Mwema, baada ya kuridhika kuwa habari hiyo
haikuwa sahihi na ilikuwa na makosa ya kitaaluma.
Kabla ya kuanza kuhojiwa, mwandishi Isango alikwenda kufanyiwa upekuzi
nyumbani kwake, ambapo maofisa wa polisi kutoka kitengo cha uchunguzi
makao makuu kwa kushirikiana na wale wa kikosi maalumu (Task Force) wa
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, walichukua vitu mbalimbali kwa ajili ya
kuwasaidia katika uchunguzi wao.
Hatua hiyo ya polisi imekuja huku kukiwa na taarifa kwamba kunafanyika
juhudi kubwa za kutaka kulifungia gazeti hili, kwa madai ya kuandika
habari zinazoichonganisha serikali na wananchi.
Mmoja wa maofisa wa Ikulu (jina linahifadhiwa) alisikika akimwambia
mmoja wa maofisa wa Kampuni ya Free Media Ltd kwamba serikali
haifurahishwi na uandishi wa habari wa gazeti hili, na akaapa kuwa
lazima Rais Jakaya Kikwete alifungie kabla ya mwaka 2015, na ikiwa
atashindwa basi yule ajaye atafanya hivyo.
Aidha, kuna habari kwamba Idara ya Habari (MAELEZO), nayo imeanza
kuhoji mambo kadhaa yanayomhusu Dk. Mbowe, ikiwa ni pamoja na kutumia
elimu yake ya udaktari wa binadamu kumiliki chombo cha habari.
Taarifa ya kusakwa kwa Dk. Mbowe ilitolewa jana wakati Misango na
Isango wakiongozwa na mwandishi wa habari hizi walipofika jana makao
makuu ya Jeshi la Polisi kama walivyotakiwa na ofisa wa juu ya jeshi
hilo, Mbuta, aliyewataka kusaidia kufanikisha kupatikana kwa mkurugenzi
wao kabla ya Ijumaa wiki hii.
“Nasikia mkurugenzi wenu ni Dk. Lilian Mbowe, naye tunamhitaji hapa
kwa ajili ya mahojiano, hivyo tunaomba msaidie apatikane maana tunataka
kupata taarifa zake kisha kupeleka kwa wakubwa kwa ajili ya hatua
zaidi,” alisema Mbuta.
Msemji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso, alipoulizwa sababu za
kumtafuta Dk. Mbowe, alisema hana taarifa, kwa kuwa tangu asubuhi ya
jana alikuwa kwenye kikao, kisha katika msafara, na kuahidi kufuatilia
baada ya kumalizika kwa shughuli hizo.
Matukio hayo yamezidi kuleta ‘sintofahamu’ ya kile kilicholengwa na
serikali dhidi ya gazeti hili, ambalo kwa sasa limetajwa kuwa kero kwa
baadhi ya watendaji wa serikali. Kadhalika, gazeti hili limekuwa
likichukuliwa kuwa mali ya chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, ambacho
kimegeuka kuwa mwiba dhidi ya serikali na CCM.
No comments:
Post a Comment