Saturday, February 2, 2013

ALBINO AUAWA, AKATWA MKONO

Thomas Murugwa, Urambo

MKAZI wa Kitongoji cha Kinondoni, Wilaya ya Urambo mkoani Tabora, Zengabuyaga Meli, ameuawa kwa kukatwa mapanga, wakati akijaribu kumwokoa mjukuu wake, Lugolola Bunzari (albino) ambaye naye alifariki baada ya wahalifu kumkata mkono na kuondoka nao.
 
  Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Anthony Rutta, wahalifu hao walivamia nyumbani kwa baba wa albino huyo, Bunzari Shinga na kuvunja mlango kisha kumkata mkono wa kushoto karibu na bega mtoto huyo mwenye ulemavu wa ngozi na kuondoka nao.
 
  Alisema kuwa kabla ya kuondoka na kiungo hicho, walimjeruhi kwa mapanga sehemu mbalimbali za kichwani, sikioni na mguuni hali iliyomfanya kutokwa na damu nyingi na hivyo kupoteza maisha.
 
  Kamanda alifafanua kuwa, watu hao pia walimuua kwa kumcharanga mapanga babu wa mtoto huyo, Zengabuyaga wakati akijaribu kumnusuru mjukuu wake.
 
  Rutta alisema kuwa watu hao zaidi ya wanane ambao bado hawajafahamika, wakiwa na silaha aina ya gobole na mapanga walivamia nyumbani kwa Shinga katika Kitongoji cha Kinondoni na kufanya mauaji hayo.
 
  Aliongeza kuwa katika mauaji hayo ambayo inadaiwa yametokana na imani za kishirikina, wauaji pia walimjeruhi sehemu ya nyonga mguu wa kulia kwa risasi baba wa mtoto huyo, Shinga ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Kitete.
 
  Kamanda alisema kuwa babu wa mtoto huyo alikatwa sehemu za sikio, mguu wa kulia na mkono wa kulia na kuachwa ukining’inia katika purukushani za kumsaidia mjukuu wake asiuawe.
 
  Pia katika tukio hilo lililotokea saa kumi ya usiku wa kuamkia juzi, wahalifu hao walimjeruhi kwa mapanga sehemu ya mguu wa kushoto bibi wa mtoto huyo, Dama Zenga ambaye naye amelazwa hospitali ya Kitete.
 
  Kamanda Rutta alisema kuwa chanzo cha mauaji hayo ya kusikitisha ni imani za kishirikina, na kwamba familia hiyo inaishi porini jambo ambalo lilikuwa gumu kwa jirani zao kutoa msaada kwa urahisi wakati walipopiga kelele.

No comments:

Post a Comment