RAIS Jakaya Kikwete jana alizindua matokeo ya awali ya Sensa ya
Watu na Makazi ya mwaka 2012, yanayoonyesha kuwa Tanzania sasa ina watu
44,929,002, kati yao 43,625,434 wakiwa wa Tanzania Bara na 1,303,568
Zanzibar.
Akitangaza matokeo ya Sensa katika Viwanja vya
Mnazi Mmoja jana, Rais Kikwete alisema takwimu hizo zinaonyesha kuwa
Tanzania ina kasi kubwa ya ongezeko la watu.
“Kwa kasi hii, hadi kufikia mwaka 2016 tutakuwa
jumla ya watu 51 milioni. Idadi hiyo yaweza kuonekana kuwa haina tatizo
kwa nchi kama Tanzania, lakini huo ni mzigo kwa taifa, jamii na kwa
uchumi,” alisema.
Alisema kuwa kwa kasi hiyo ya ongezeko la watu
hapana budi kuwa na mikakati madhubuti na mipango mipya ya maendeleo
kuanzia sasa.
“Kuna umuhimu wa kupanga uzazi, vinginevyo hali ya
maisha itazidi kushuka na ushindani katika rasilimali hizi chache
tulizonazo utazidi kuwa mkubwa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Lazima tulipe uzito stahiki suala hili la kupanga
uzazi. Lazima ujue utazaa kipindi gani na watoto wangapi ili uweze
kuwahudumia.”
Alisema takwimu za matokeo hayo zina maana kwamba
Serikali ianze kujipanga kwa ongezeko hilo la watu na jamii kwa upande
wake, ianze kujipanga kukabiliana nalo.
“Tukizingatia haya tutaweza kupiga hatua. Sisi
serikalini tutaanza kupanga mipango yetu kwa kuzingatia matokeo haya.
Nanyi wenzangu anzeni kujipanga kuchukua hatua,” alisema Rais Kikwete.
Alisema matokeo mengine yatatolewa Februari ambayo ndiyo yataonyesha mchanganuo wa jinsia, umri kiwilaya, kikata na kishehia.
Rais Kikwete alisema Sensa ya mwaka 2012, ni ya
tano kwa Tanzania, ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 na kulikuwa na watu
12,313,054; Tanzania Bara watu 11,958,654 na Zanzibar 354,400.
Sensa ya mwaka 2002 ilionyesha kuwa Tanzania ina
zaidi ya watu 34 milioni. Alisema tangu Sensa ya kwanza ilipofanyika
hadi ya sasa, kuna ongezeko la watu zaidi ya 33 milioni.
Alisema hatua ya mwisho ya matokeo ya Sensa ya
2012 yanatarajiwa kutolewa Juni, 2013 ikiwa na mchanganuo wa taarifa
zote muhimu zikiwamo za kiuchumi kwa kaya.
No comments:
Post a Comment