JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema askari anayedaiwa
kuwa jeshi hilo aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),
Godbless Lema ametoroka.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema
jana kwamba pamoja na hatua yake ya kutoroka, jeshi litaendelea kumsaka
kwa udi na uvumba ili kumhoji na kujiridhisha kama kweli ni mwanajeshi
wake kabla ya kumchukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kifungu cha
147 cha Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya 1977.
“Huyu kijana inasemekana alishawahi kupitia Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT), lakini wakati tunaendelea na uchunguzi alitoroka
katika nyumba aliyokuwa amepanga bila ya taarifa kwa baba mwenye
nyumba,” alisema Kanali Mgawe na kuongeza:
“Askari huyo alikuwa anaishi katika nyumba ya
kupanga mita chache karibu na Kituo cha Polisi cha Simanjiro, Arusha na
alikuwa akijishirikisha na ulinzi shirikishi.”
Alipoulizwa jina la askari huyo, Kanali Mgawe alijibu: “Yeye alikuwa anafahamika mtaani hapo kwa jina la kamanda.”
Hata hivyo, Kanali Mgawe alisema jeshi hilo
litahakikisha linatoa ripoti kamili kwa umma baada ya kumkamata na
uchunguzi kukamilika ili kuondoa utata uliogubika suala hilo.
Alipoulizwa kama kuna tofauti gani kati ya mwanajeshi kuingia kwenye mikutano ya wanasiasa na wale wanaofanya kazi za kisiasa kama wakuu wa wilaya na mikoa, Kanali Mgawe alijibu:” Wanajeshi wanaofanya kazi za U-DC au RC, wanaruhusiwa kisheria.”
Alipoulizwa kama kuna tofauti gani kati ya mwanajeshi kuingia kwenye mikutano ya wanasiasa na wale wanaofanya kazi za kisiasa kama wakuu wa wilaya na mikoa, Kanali Mgawe alijibu:” Wanajeshi wanaofanya kazi za U-DC au RC, wanaruhusiwa kisheria.”
Alifafanua kuwa iwapo mwanajeshi atateuliwa
kufanya kazi katika taasisi yeyote ya Serikali nje ya jeshi, atatakiwa
kuvua magwanda ya jeshi na kufanya kazi hiyo mpaka atakapomaliza muda
wake na baada ya hapo ataruhusiwa kurejea jeshini.
“Kuna kitu kinaitwa ‘secondment.’ Mwanajeshi
anaruhusiwa kufanya shughuli zozote nje ya jeshi iwapo atahitajika
kufanya hivyo. Ila kwa masharti ya kuvua magwanda, hivyo wananchi
wasishangae kuwaona baadhi ya askari wetu ni wakuu wa wilaya na mikoa na
baadaye kurudi jeshini kuendelea na majukumu yao,” alisema Kanali Mgawe
na kuongeza:
“Askari akiwa katika majukumu yake mapya, atafanya
kazi zote atakazopewa zikiwamo za kisiasa kama ilivyo kwa wakuu wa
wilaya na mikoa, lakini akirudi jeshini, anarudi kuwa askari mwenye utii
na kufuata kanuni za jeshi zisizofungamana na siasa.”
No comments:
Post a Comment