Thursday, November 15, 2012

MAKETE WAANZA KUNUFAIKA NA PARETO

Wananchi wa kijiji cha Ugabwa wilayani Makete wamesema zao la pareto limekuwa msaada mkubwa kwao mara baada ya serikali kuwapatia mbegu za zao hilo na wao kukubali kulilima

Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo wananchi hao wamesema zao hilo lilianza kulimwa na kusimamiwa na kikundi kilichoundwa miaka miwili iliyopita ambapo kwa sasa kila mwanakikundi analima katika mashamba yake

Wamesema kutokana na zao hilo kuwa na bei kubwa sokoni ya sh.2,200/= kwa kilo moja, hawana budi kuendelea kulima pareto kwa kuwa wanaona faida yake

Kwa upande wake mhasibu wa kikundi cha pareto kijijini hapo Bw. Alpha Mahenge amesema zao hilo linawasaidia kujikwamua na changamoto mbalimbali ikiwemo kuwatimizia mahitaji watoto wao ambao ni wanafunzi pamoja na kutunza familia

Katika hatua nyingine katibu wa kikundi hicho Bw. Ezekiel Mahenge amesema serikali imewapa mbegu kwa ajili ya kuotesha na miche hiyo wataigawa kwa wanakikundi ili wakaioteshe kwenye mashamba yao

Naye mwenyekiti wa kijiji hicho Bi. Rose Chaula ameishukuru serikali kwa kutambua kwa kuwahimiza wanaugabwa kulima pareto pamoja na wananchi wa kijiji chake kukubali kulima zao hilo na kuahidi kuendelea kuwahimiza wananchi wote kulima pareto
Na Furahisha Nundu

No comments:

Post a Comment