Monday, December 2, 2013

WAMBULA AJITOA SIMBA

Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) sasa TFF, Michael Wambura amejitosa kuvalia njuga mgogoro wa Simba unaoendelea na kudai kuwa amekubaliana na uteuzi wa ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba aliyoteuliwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage.
Akizungumza Makao Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi, jana, Wambura alisema kwa mujibu wa Katiba ya Simba Ibara ya 28(1)(d) Mwenyekiti anaweza kuteua wajumbe wawili kuingia kwenye Kamati ya Utendaji ya Simba bila kutoa nafasi ya wateuliwa kuuliza wameteuliwa kutoka katika kundi lipi kati ya wajumbe wawili.
“Nadhani jambo muhimu la kuhoji ni wanaoteuliwa wanakwenda kufanya nini kwenye Kamati ya Utendaji kwa maana ya uwezo wao kuisaidia Simba na sio nani ateuliwe na nani asiteuliwe kwani hilo liko katika mamlaka ya mteuzi ilimradi tu anayeteuliwa ni mwanachma wa Simba na ataongeza tija kwa klabu, alisema Wambura.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Wambura imepingwa na Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Swedy Nkwabi ambaye alidai kuwa uteuzi wa Wambura kikatiba sio sahihi na kumshangaa Wambura kuzungumzia mgogoro wao wakati hawakukubaliana naye.
“He! Yaani alituuliza kumbe lengo lake lilikuwa ni kuongea na vyombo vya habari, mimi nilijua ameuliza tu kutaka kufahamu na nilichukulia ushauri wake kuwa ni mzuri ila sikufahamu lengo lake hasa ni nini, nasemaje uteuzi wake kikatiba si sahihi na wala hatukubaliani na uteuzi huo, na pili nitakutana na wenzangu kuzungumzia jambo hili na tutalitolea tamko,” alisema Nkwabi.
“Ninaamini uzoefu wangu katika uongozi wa mpira wa miguu na elimu yangu ulifaa kuingia katika Kamati ya Utendaji ya Simba, alisema Wambura.
“Nilipata nafasi ya kuongea na Mwenyekiti  wa Simba na kisha kuongea na mjumbe mmoja mmoja wa Kamati ya Utendaji ili kujua kiini na sababu za sintofahamu iliyokuwa inaendelea ndani ya uongozi wa Simba, wajumbe walikuwa na masikitiko na manung’uniko ya msingi ambayo Mwenyekiti atakaporejea atakutana na kamati yake ili mamabo ya msingi yaliyozungumzwa yafanyiwe kazi na kupanga utekelezaji wake. Mwenyekiti ameisha taarifiwa juu ya auamuzi huu,” alisema.

No comments:

Post a Comment