Monday, December 2, 2013

DK KITILA ASIMAMISHWA UONGOZI UDSM

Siku chache baada ya Dk Kitila Mkumbo kuvuliwa ujumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nao umemsimamisha kuongoza Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce).
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Yunus Mgaya alisema Dk Kitila amesimamishwa kwa muda usiojulikana baada ya uongozi kupata taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa ni kiongozi wa Chadema wakati akiwa mtumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi.
Profesa Mgaya alisema Dk Kitila alipewa barua ya kusimamishwa Ijumaa iliyopita na sasa atabakia kuwa mhadhiri mwandamizi kwenye kitivo hicho.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Dk Kitila alikiri kupokea barua ya kusimamishwa wadhifa wa Mkuu wa Kitivo cha Elimu.
“Ni kweli nimepokea barua ya kusimamishwa lakini kwa sasa siwezi kuzungumza zaidi,” alisema Dk Kitila.
Profesa Mgaya alisema UDSM kilikuwa kinafahamu kuwa Dk Kitila alikuwa mwanachama wa kawaida wa Chadema na siyo kiongozi. Alisema uongozi wa chuo hicho utaunda timu maalumu ya kuchunguza suala hilo na itaanza kazi mara moja.
Profesa Mgaya alisema timu hiyo itakuwa na kazi mbili, kwanza kuchunguza kama kweli Dk Kitila alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na kisha kupata maelezo ya Dk Kitila juu ya suala hilo.
Hivi karibuni, Dk Kitila na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe walivuliwa nyadhifa zao zote ndani ya chama hicho kwa madai ya kuandaa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 kinyume cha itifaki na sheria za chama hicho.
“Tumemsimamisha (Dk Kitila), ili kupisha uchunguzi, tunataka tujiridhishe na yale yanayoandikwa na vyombo vya habari, pia kumpa nafasi ya kujitetea, hatuwezi kumsimamisha tu na kukaa kimya, tunataka kufanya mambo kisheria,” alisema Profesa Mgaya.
“Timu yetu itakwenda huko Chadema kupata taarifa zaidi na Dk Mkumbo pia atasikilizwa,” alisema Profesa Mgaya na kuongeza kuwa timu hiyo itafanya kazi yake ndani ya muda mfupi na matokeo ya uchunguzi wake ndiyo yatakayoamua hatima yake.
Dk Kitila kusimamishwa Chadema
Kamati Kuu ya Chadema ilikutana Dar es Salaam Novemba 20 na 21 na kuamua kuwavua uongozi, Dk Mkumbo, Zitto na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba baada ya kuwatuhumu kuhusika kuandaa waraka huo ambao ulilenga kuhamasisha mabadiliko makubwa katika uongozi wa ngazi ya juu ya chama hicho katika uchaguzi wake mkuu ambao umepangwa kufanyika Juni mwakani.

No comments:

Post a Comment