WAKATI
nchi ikiendelea kuandamwa na zimwi la kuporomoka kwa majengo, Tanzania
Daima Jumapili limebaini udhaifu mkubwa kwenye Bodi ya Makandarasi
(CRB).
Uchunguzi umebaini kuwa takribani wiki mbili, umejiridhisha
pasipo shaka kwamba CRB imeisajili Kampuni ya Visual Storm Co. Ltd kwa
kutumia nyaraka bandia na imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa bila
kuisajili kwenye bodi hiyo kama sheria inavyosema.
Kampuni hiyo inamilikiwa na Noel Severe (30), mtoto wa mkurugenzi wa
zamani wa wanyamapori, Emmanuel Seveve ambaye wakati fulani aliingia
kwenye mgogoro wa kiuongozi wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Anthony
Diallo.
Severe ni mkwe wa waziri mkuu aliyejiuzulu ambaye pia ni mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa ambaye amemuoa bintiye aitwaye Dk. Adda Lowassa.
Katika kile kinachoonyesha kuwepo kwa nguvu ya viongozi nyuma ya
pazia, Visual Storm iliweza kupewa mkataba wa ukarabati wa tawi la Benki
ya Biashara ya Dar es Salaam (DCB) mwaka 2011 ikiwa bado haijasajiliwa
na CRB kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa nyaraka ambazo gazeti hili linazo, kampuni hiyo
ilisajiliwa kwa Msajili wa Makampuni (Brella) mwaka 2009 kwa No. 71362
na kisha CRB Februari 23, 2013 kwa No. B5/0674/2/12 daraja la tano.
Gazeti hili limebaini kuwa kabla ya usajili CRB, Visual Storm
iliingia mkataba na DCB Oktoba 3, 2011 wa kujenga ukumbi wa mikutano
katika tawi la Ukonga kwa gharama ya sh 56,676,580 kwa muda wa wiki
tano.
Hata hivyo, hadi kufikia Januari 9, 2013 zaidi ya mwaka mmoja,
kampuni hiyo ilikuwa imeshindwa kukamilisha kazi hiyo, hatua
iliyomlazimu Mkurugenzi Mkuu wa DCB, Edmund Mkwawa kuiandikia
akiitaarifu kusudio la kutaka kuvunja mkataba huo.
Nakala ya barua hiyo pia ilipelekwa kwa msajili wa CRB, Boniface
Muhegi, ambapo Februari 12, 2013, bodi hiyo kupitia kwa kaimu meneja wa
Kanda ya Mashariki, D. J. Karugendo, ilijibu kwa kuiandikia Visual Storm
na kuipa siku saba itoe maelezo ya kushindwa kutimiza mkataba huo.
Alipotafutwa Mkwawa ili kufafanua ni kwanini benki yake iliingia
mkataba na kampuni ambayo haikuwa imesajiliwa CRB, alisema kuwa suala
hilo aulizwe Visual Storm.
“Tunawasubiri hao CRB tukutane mahakamani, lakini kwanini usiwaulize Visual Storm wakakupa majibu?” alisema.
Hadi gazeti hili linafanya uchunguzi huo, CRB inadai kuwa haikuwa na
taarifa ya kasoro hiyo ya Visual Storm kuvunja sheria ya kuingia mkataba
wa ujenzi bila kusajiliwa, licha ya kupata barua ya malalamiko ya DCB.
Katika kosa hilo, Muhengi anathibitisha kuwa kampuni hiyo inapaswa
kuadhibiwa kwa kutozwa faini pamoja na DCB kwa kutoa zabuni kwa kampuni
ambayo haikuwa na usajili wa Bodi ya Makandarasi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, kampuni hiyo ililazimika kukimbilia CRB
kujisajili baada ya kushindwa kutimiza mkataba wa DCB kwa wakati, na
hivyo kuhofia kukumbwa na rungu la adhabu baada ya benki hiyo kuanza
kulalamika.
Hata hivyo, katika kujinasua, kampuni hiyo ilitumia nyaraka na
vielelezo visivyo halali, hatua ambayo Muhegi anasema itasababisha sasa
iadhibiwe kwa kufutiwa usajili wake, na wamiliki wake kuchukuliwa hatua
za kisheria.
Ili kampuni iweze kusajiliwa CRB, Muhegi anasema ni lazima itimize
vigezo kadhaa kulingana na daraja husika ambapo wamiliki wanatakiwa kuwa
na wataalamu, ofisi na vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wa wataalam, kampuni inapaswa kuwa na mkurugenzi wa ufundi
ambaye amesajiliwa na Bodi ya Mainjinia (ERB) ambaye atakuwa ameajiriwa
na kampuni husika na kuwa mmoja wa wanahisa.
Lakini katika hatua ya kushangaza, Kampuni ya Visual Storm, awali
iliwasilisha vielelezo vya vyeti vya Loserian Sokonoi ambaye hata hivyo
alitofautiana na mmiliki Severe na kuamua kuondoka na kuajiriwa
serikalini mkoani Shinyanga.
Kampuni hiyo katika kusaka usajili wa haraka, ilitumia cheti cha Kent
Kissima na kumtambulisha kama mkurugenzi wao wa ufundi ilhali mtu huyo
ni mwajiriwa wa serikali akifanya kazi kama meneja wa Wakala wa Barabara
(Tanroads) makao makuu.
Awali katika majibu yao, CRB walijikanganya wakidai mkurugenzi wa
ufundi wa kampuni hiyo ni Sokonoi, lakini walipobanwa zaidi wakadai ni
Kissima ambaye inadaiwa amehamishwa makao makuu Tanroads na kupelekwa
kuwa meneja wa Mkoa wa Simiyu.
“Mimi ninamfahamu Kissima kama ‘technical director’ wa Visual Storm
wala si Sokonoi,” alisema Muhegi lakini alipoelezwa kuwa Kissima ni
mwajiriwa na Tanroads akafichua siri kuwa kampuni hiyo vielelezo vyake
vyote vilikuwa vya kughushi.
“Tumekwenda huko TRA (Mamlaka ya Mapato) tumekuta kadi za vifaa
walizowasilisha huko sio vya kwao, kinachofuata sasa ni kuifuta na
kuanza utaratibu wa kuwasiliana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) na vyombo vingine vya kisheria,” alisema.
Hata hivyo, Muhegi alipobanwa alionyesha kuhamaki mara kadhaa na
kuhusisha suala hilo na fitna za kisiasa, akisema; “najua aliyekutuma ni
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha.”
Alipoulizwa ilikuwaje hawakujiridhisha na umiliki wa vifaa hivyo
kabla ya usajili, alitoa majibu yasiyoridhisha akisingizia kuwa bodi yao
haina mtandao wa kuweza kufuatilia makandarasi wote.
Alipotafutwa Sokonoi kuthibitisha kama ndiye bado mkurugenzi wa
ufundi wa kampuni hiyo, alijibu kwa msisitizo kuwa; “Huyo jamaa
tulifanya naye kazi, lakini wakati tukiwa kwenye mchakato huo wa usajili
alionekana kunizika fedha zangu nikajiondoa.
“Mimi kwa sasa niko Shinyanga nimeajiriwa serikalini na
nilikwishawaandikia CRB kuwaarifu kuwa vyeti vyangu visitumike popote
kwenye taasisi yao kwa namna yoyote, maana sifanyi kazi huko tena.”
Hata hivyo, katika kile kinachoonyesha udhaifu wa CRB, gazeti hili
linayo nakala ya makubaliano kati ya Visual Storm na Kampuni ya
Fabec/Home base (T) Ltd.
Makubaliano hayo yanaonyesha kuwa wakati wa kukaguliwa vifaa vya
ujenzi, Visual walionyesha kwa CRB mkataba huo wakidai vifaa vyao
wameikodishia Fabec iliyokuwa na kazi ya ujenzi wa barabara ya
Sumbawanga-Mpanda wakati huo.
Msemaji wa Fabec, Ziota, alipotafutwa alilieleza gazeti hili kuwa kampuni yao haijawahi kuwa na mkataba wa aina hiyo na Visual.
“Kampuni hiyo wala sijawahi kuisikia, inamilikiwa na nani?” alihoji
Ziota na kufafanua kuwa hata kama wangekuwa wamekodishwa vifaa hivyo,
CRB walitakiwa kutembelea mradi wao kujiridhisha kama vipo kweli.
Hata baada ya kusajiliwa CRB, Kampuni ya Visual Storm imeendelea
kutekeleza miradi yake mikubwa ikiwemo ile ya Shirika la Taifa la
Hifadhi ya Jamii (NSSF) bila kuisajili kwenye Bodi ya Makandarasi kama
sheria inavyosema wala kufuata taratibu za kuwa na vibali vya ujenzi.
Severe ajitetea
Alipotafutwa kujibu tuhuma hizo, Mkurugenzi Mkuu wa Visual Storm,
Severe alikiri na kuonyesha mshangao akihoji nani alivujisha suala hilo
kwenye vyombo vya habari.
Alidai kuwa ameshangaa kuona nyaraka sahihi alizompatia mshirika wake
kwa ajili ya kushugulikia usajili, zilibadilishwa na kupachikwa zile za
kughushi.
“Kaka yaani nashangaa kwanini jambo hili linakuwa hivi, mimi hivi
vifaa unavyonionyesha hapa kampuni yetu haina na sijui hawa walivitoa
wapi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu utata wa mkurugenzi wao wa ufundi, Severe alimtaja
Sokonoi kuwa ndiye waliyewasilisha jina lake CRB. Lakini alipobanwa
aeleze inakuwaje mhusika anafanya kazi serikalini, alisema walikuwa
kwenye mkakati wa kumbadilisha.
Alipoelezwa kuwa CRB wamedai wanamtambua Kissima kama mkugenzi wa
ufundi wa kampuni hiyo, Severe alidai kutomtambua mtu huyo huku
akionyesha kushangaa alichomekwaje na kuwa mmoja wa wanahisa.
Severe katika kujitetea alimtwisha lawama mtu aliyemtaja kwa jina la
Ruben ambaye alidai kuwa alikuwa mshirika wake kuwa ndiye alivujisha
siri hiyo kwa sababu wakati wa usajili CRB alihusishwa kwa ukaribu.
Tanzania Daima lilimtafuta Emmanuel Ruben, ambaye alikiri
kushirikiana na Severe katika usajili wa kampuni hiyo CRB, lakini
akasema kuwa baadaye walihitilafiana katika mgawanyo wa rasilimali na
hivyo akajitoa na kuanzisha kampuni yake.
“Mimi pale CRB nina power of attorney (nguvu ya kisheria) kwa kampuni
ya Visual Storm kwa vile tulikuwa pamoja, lakini kwa sasa niko
kivyangu, sasa hayo ya kwamba nimeleta siri hiyo kwenu ndiyo nasikia
kwako,” alisema Ruben.
No comments:
Post a Comment