Ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Arusha zimenusurika kuteketea baada ya watu wasiojulikana kuwasha moto katika moja ya vyumba vyake jana alfajiri.
Wakati hayo yakitokea, msuguano ndani ya chama
hicho umeendelea kushika kasi baada ya jana, Mwenyekiti wake Mkoa wa
Singida, Wilfred Kitundu kujiuzulu akipinga hatua ya Kamati Kuu kumvua
nyadhifa zake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe.
Moto Arusha
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alisema jana kwamba walipata taarifa za kuungua kwa ofisi hizo zilizopo
eneo la Ngarenaro saa mbili asubuhi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Aman Golugwa
alisema chumba cha kompyuta ambacho kina kumbukumbu za wanachama wote
Kanda ya Kaskazini kimeathirika.
“Hii ni hujuma dhidi ya Chadema; watu hawa
walipanda juu ya ukuta na kuingia ndani kupitia kwenye dari kisha
kuchoma moto ofisi,” alisema Golugwa.
Alisema vyumba viwili ndivyo, vimeungua kabisa na
kwa bahati nzuri moto ulishindwa kusambaa na kuzimika baada ya umeme
kuzimwa. Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Wilaya ya
Arusha, Happiness Chale ambaye aliwahi kushuhudia tukio hilo alisema,
mhudumu wa ofisi hiyo, Jenipha Mwacha alibaini moto huo baada ya
kusambaa na kufika katika maliwato. Alisema kwa kawaida ofisi hiyo
inalindwa na walinzi wa Red Brigade.
Polisi walifika mapema eneo hilo na kuweka uzio
ili kuzuia watu kuingia katika ofisi hizo pamoja na kuanza uchunguzi wa
tukio hilo.
Wakati polisi wakiwa katika ofisi hizo, viongozi
wa Chadema Mkoa na Wilaya ya Arusha walikuwa wakitoa maelezo polisi
kuhusiana na tukio hilo.
Mwenyekiti Singida
Huko Singida, Kitundu amejiuzulu nafasi hiyo jana huku akieleza kuwa chama hicho kinakiuka misingi ya demokrasia.
Uamuzi wa Kitundu umekuja siku nne tu, tangu
Mwenyekiti wa Chadema mkoani Lindi, Ally Chitanda naye kujiondoa katika
nafasi hiyo akieleza kuchoshwa na uamuzi wa kikanda na kikabila
unaoendelea ndani ya chama hicho.
No comments:
Post a Comment