WAKATI
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikimwandikia Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe barua ya kumtaka ajieleze dhidi ya tuhuma
zinazomkabili, yeye ameamua kukimbilia polisi akimshitaki mmoja wa
viongozi wenzake; Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari za kuaminika zimedai kuwa Zitto ambaye hivi karibuni alivuliwa
cheo chake cha unaibu katibu mkuu wa CHADEMA, inadaiwa amefungua
mashitaka polisi akimtuhumu Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam,
Henry Kileo kwa madai ya kusambaza waraka katika mitandao ya kijamii.
Akithibitisha tukio hilo, wakili wa Kileo, Peter Kibatara, alisema
kuwa mteja wake amemriwa kufika makao makuu ya Jeshi la Polisi leo
Jumatano saa nane mchana na kuonana na mmoja wa maofisa wa juu wa jeshi
hilo, aliyetajwa kwa jina moja tu la Mbutta, kufuatia mashitaka
yaliyofunguliwa na Zitto dhidi yake.
Hata hivyo, Kibatara hakusema waraka huo unasema nini, na kwa nini
hali hiyo inatokea kwa sasa katika kipindi ambacho Zitto anakabiliwa na
tuhuma za usaliti ndani ya chama chake.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima Jumatano, Kileo
alikiri kuitwa polisi, ingawa alidai hajui ni waraka gani anaotuhumiwa
kuusambaza unaomchafua Zitto.
“Kwa kweli sijui hata mimi ni waraka gani, ingawa hivi karibuni
kulikuwa na waraka wa siri uliodaiwa kutoka CHADEMA, na ambao ulijaa
tuhuma za usaliti. Lakini huo tuliishaukana siku nyingi. Labda kuna
mwingine,” alisema Kileo.
Zitto kutwa nzima ya jana hakuweza kupatikana kwa njia ya simu
kufafanua mashitaka aliyofungua polisi. Simu zake zote za kiganjani
zilikuwa zimezimwa.
Jana, CHADEMA kupitia kwa mwanasheria wake mkuu, Tundu Lissu, ilijibu
hoja zilizotolewa na Zitto pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu,
Dk. Kitila Mkumbo mbele ya waandishi wa habari na kudai kuwa viongozi
hao wanakabiliwa na tuhuma 11 wanazotakiwa kuzijibu.
Akizungumza katika makao makuu ya chama hicho, Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi, John Mnyika, alisema Zitto na Kitila wameandikiwa barua za
kujibu tuhuma hizo na kwamba watapewa wakati wowote kuanzia leo (jana).
Kuhusiana na kile kilichoelezwa na Zitto na Dk. Kitila, Wakili Lissu
alisema kuwa mkutano uliofanywa na viongozi hao waliovuliwa madaraka
mbele ya waandishi walishindwa kusema ukweli wa kile kilichowafanya
wavuliwe nafasi zao.
Lissu alisema Zitto na Dk. Kitila hawakusimamishwa nyadhifa zao kwa
masuala ya PAC, uchaguzi wa mwaka 2010, wala kutoshiriki kwenye
operesheni za chama au sababu zingine, na walitaja hizo sababu ili
kupotosha tuhuma zinazowakabili kwa jamii.
“Walichokifanya kina Zitto na Kitila ni “Diversion” (kubadili
mwelekeo) wa mashitaka yao yanayotokana na waraka wa kihaini wa
mabadiliko, ambao ni kinyume na katiba, kanuni na maadili na itifaki ya
chama. anawaambia waandishi,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa CHADEMA kina mwongozo wa uchaguzi uliopitishwa na
Kamati Kuu, Zitto na Kitila wanaufahamu ingawa haijulikani ni kwanini
wao walienda kinyume na mambo yanayojadiliwa katika Kamati Kuu.
Aidha, Lissu alieleza kuwa Dk. Kitila anapotosha umma kwa kauli yake
kuwa Kamati Kuu haina mamlaka ya kumvua nafasi yake ya ujumbe wa Kamati
Kuu maana amechaguliwa na Baraza Kuu.
Aliwataka waangalie vema katiba ya chama, hasa majukumu ya Kamati
Kuu, pale yanaporuhusu mwanachama yeyote kusimamishwa au kufutiwa
uanachama kama Kamati Kuu itaona kuna umuhimu wa kufanya vile.
Alisema Zitto alipaswa kumkumbusha Dk. Kitila kuhusu suala hilo maana
mbunge huyo alikuwepo kwenye Kamati Kuu iliyomvua ukatibu mkuu Dk.
Walid Kabour, na makamu mwenyekiti bara, Chacha Wangwe.
Akaongeza kuwa kama Kamati Kuu iliweza kwa Kabour na Wangwe, imeweza
na kwake pia ambaye kwa cheo ni mdogo kuliko Katibu Mkuu au Makamu
Mwenyekiti.
CHADEMA yajipanga
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Oganaizesheni na
Mafunzo, Benson Kigaila, alisema programu ya sasa ya ujenzi wa chama
hicho toka makao makuu kwenda ngazi ya kanda iliyopitishwa Januari 28,
mwaka huu iliunda kanda ili kugatua madaraka.
Mkakati huo ulianza na kuzindua kanda na uongozi wa kanda, kutoa
mafunzo kwa timu za taifa, kanda, mikoa, majimbo, kata, vijiji/mitaa na
vitongoji, hatua ya tatu kuunda msingi ya chama na mwisho itakuwa ni
kufanya uchaguzi wa ndani ya chama.
Kwa mujibu wa Kigaila, kanda zote nane za bara zimekwishazinduliwa na
zina uongozi kamili, na upande wa Zanzibar mkakati huo utazinduliwa
Desemba.
Aidha kuhusu timu ya mafunzo, Kigaila alisema kuwa kitaifa kuna
wakufunzi 10, kikanda wapo 40, kimajimbo 956, kwa ngazi ya kata 19,408,
na kwenye vijiji na mitaa kuna wakufunzi 72,000.
Kigaila alisema sasa CHADEMA imetuma timu 13 zinazoondoka makao makuu
kwenda katika kanda kushirikiana na timu nyingine ili kuunda timu 103
za majimboni kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa zoezi hili, kutambua
changamoto zilizopo na kusaidia na kupata suluhisho, pamoja na kazi ya
kutoa mafunzo juu ya katiba ya chama, kanuni za chama na usimamizi wa
uchaguzi kwa ngazi zote.
No comments:
Post a Comment