Tuesday, November 26, 2013

RAIA WA NAIGERIA AKAMATWA NA UNGA KIA

JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro kitengo cha dawa za kulevya
limemnasa  raia wa Nigeria, Chubuzo John,
akiwa na dawa za kulevya zinazokadiriwa kuwa na uzito wa kilo
nne katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk.
Harrison Mwakyembe, kutoa onyo kali kwa maofisa wa umma katika uwanja
huo kuufanya kuwa njia ya kupitishia dawa za kulevya baada ya
kufanikiwa kudhibiti Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, aliiambia Tanzania Daima kwa njia ya simu akiwa safarini kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa majira ya
saa 11:45 jioni wakati wa ukaguzi wa mizigo akiwa amebeba dawa hizo
kwenye mizigo yake akielekea nchini Italia.
Boaz alisema Chubuzo akiwa uwanjani hapo alikuwa akifanya maandalizi
ya kusafirisha mzigo huo kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopian Airline kuelekea jijini Roma, Italia.
“Huko KIA raia huyo wa Nigeria, Chibuso John, alikamatwa wakati akitaka
kuondoka kwa kutumia  ndege ya Shirika la Ethiopian Airline kwenda
Roma, Italia…tayari hizo dawa tumempelekea Kamishna wa Dawa za Kulevya, yeye ndiye atakayesema kwamba  thamani yake ni kiasi gani na ni aina gani
ya dawa alizokamatwa nazo,” alisema Boaz.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini
mtandao wa mtuhumiwa huyo kabla ya kumpeleka mahakamani kusomewa
mashitaka yanayomkabili kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hivi karibuni Waziri Mwakyembe alifanya ziara ya kushtukiza katika
uwanja huo huku akitoa onyo kwa maofisa wa idara za usalama pamoja na
maofisa wa umma kutojiingiza katika mtego wa kuugeuza Uwanja wa KIA
mapitio ya dawa za kulevya kwani siku zao zinahesabika.
Mwakyembe alisema anatambua wafanyabiashara wa dawa za kulevya
wanautumia Uwanja wa KIA kama njia ya kusafirisha kwenda ughaibuni baada ya ule wa Mwalimu Nyerere kudhibitiwa.

No comments:

Post a Comment