Wednesday, November 27, 2013

MARUFUKU KUUZA VISU NA SIME BARABARANI

 

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imepiga marufuku biashara ya kutembeza visu, sime na mapanga barabarani na kusema yeyote atakayekiuka agizo hilo atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema jeshi hilo lipo katika mchakato wa kupendekeza sheria mpya ya matumizi ya silaha na umiliki ili kudhibiti matumizi mabaya yakiwamo uuzaji wa visu, mapanga na sime kiholela.
Kamishna Kova alisema tatizo kubwa si mtu kumiliki silaha, bali jinsi watu wanavyozitumia vibaya na kusababisha madhara katika jamii na kuongeza kuwa sheria hiyo itajumuisha uuzaji holela wa visu, mapanga na sime barabarani na umiliki wa silaha za  moto.
“Kwa mfano visu, kwa kawaida vinatumiwa nyumbani kukatia nyanya na vitunguu, lakini mtu anaweza kukitumia vibaya kwa kumchoma nacho mtu tumboni au kifuani...hivyo atakayeonekana anauza vitu hivyo, atachukuliwa hatua.
 Hatua hiyo imekuja baada ya mfululizo wa mauaji ya kutumia silaha za moto yanayohusishwa na wivu wa mapenzi kukithiri nchini.
Novemba 19, mwaka huu, Gabriel Munisi aliwaua watu wawili kwa risasi na kumjeruhi mpenzi wake, Christina Newa, mama mzazi wa mpenzi wake, Ellen Eliezer na kisha kujiua, kwa kile kinachoaminika kuwa ni wivu wa mapenzi.
Mapema Oktoba mwaka huu, Mwandishi wa Habari wa Kituo cha ITV, Ufoo Saro alijeruhiwa pia kwa risasi na mpenzi wake, Anthery Mushi. Pia alimuua mama mzazi wa Ufoo na kisha kujiua kwa kujipiga risasi.
Kamishna Kova alisema pia kuwa katika mchakato huo wa kuunda sheria mpya za umiliki wa silaha, hatua kali ikiwamo kunyang’anywa silaha hizo kwa watu wanaozitumia vibaya itachukuliwa.
Hata hivyo, alisema wakati sheria hizo zikisubiriwa, polisi watawachukulia hatua kali wote watakaobainika kuzitumia vibaya. Aliwataka Watanzania kuwa makini na matukio ya uhalifu katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na sikukuu.

No comments:

Post a Comment