Tuesday, July 30, 2013

MADIWANI WAMGEUKIA KIKWETE


     

MADIWANI wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Manispaa ya Bukoba, wamemgeuka Rais Jakaya Kikwete, wakawasilisha barua kwa mkurugenzi wa manispaa hiyo, kumtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kutokuwa na imani na meya anayetuhumiwa kujiingiza katika miradi ya kifisadi.

 Wameungana na wenzao wanne wa CHADEMA na watatu wa CUF kuchukua uamuzi huo baada ya siku tatu tangu Rais Kikwete alipoamuru wapatane na meya, Anatory Amani, ambaye amekuwa katika mgogoro na Mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki.

 Huku akijua kuwa mgogoro wao haukuwa wa watu binafsi bali maslahi ya wananchi wa Bukoba, Rais Kikwete aliwataka mbunge na meya “waondoe tofauti zao.” Madiwani wamepinga kauli hiyo wakisema suluhu ni kupinga ufisadi wa meya, kwani hakuna ugomvi binafsi kati yake na mbunge.

 Akihutubia mkutano katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Jumapili iliyopita,  Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko kuu la kisasa katika manispaa hiyo lazima uendelee na kwamba hakuna hoja ya kuendelea na malumbano “yasiyokuwa na msingi.”

 Madiwani hao 15 walisema malumbano yaliyopo ni ya msingi kwa kuwa watu watakaobebeshwa deni la kurejesha mikopo inayochukuliwa na meya ni wakazi wa Bukoba, si meya mwenyewe.

 Walisema rais ameonekana hafahamu kiini cha mgogoro, kwani kinachopingwa si miradi, bali utaratibu ambao meya ametumia kuanzisha miradi hiyo kifisadi bila kuzingatia maslahi ya wananchi.

 Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhama ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.

 Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.

 Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.

 Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.

 Barua ya madiwani hao iliwasilishwa jana asubuhi saa 2.30 na kupokelewa na Mkurugenzi wa Manispaa, Shimwela L.E, ikiwa na saini za madiwani 16 kati ya 24 waliopo.

 Hata hivyo, mkurugenzi huyo, alipotafutwa na gazeti hili alishindwa kukiri au kukanusha kupokea barua hiyo, akisingizia kuwa kwa muda huo alikuwa akitekeleza majukumu yake nje ya ofisi.

 “Unajua rais juzi ameacha maagizo mengi na baya zaidi ni lile la ugawaji wa viwanja, hivyo asubuhi niliingia ofisini na kutoka kuelekea mitaani. Nitakupa taarifa kesho kama barua hiyo imefika,” alisema.

 Kwa mujibu wa kanuni za manispaa hiyo yenye madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM, ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.

 Kanuni hizo pia zinaelekeza kuwa mkurugenzi atapaswa kuitisha kikao hicho ndani ya siku saba kuanzia tarehe aliyopokea barua ya tuhuma hizo za madiwani na ndani ya muda huo anapaswa kuwa amempatia mtuhumiwa tuhuma hizo ili aweze kuzijibu.

 Akithibitisha kuwasilishwa kwa barua yao hiyo, mmoja wa madiwani hao, Richard Gaspar (CCM) wa Kata ya Miembeni alisema kuwa awali walikuwa wamesaini madiwani 16 lakini wameamua kumtoa Balozi Kagasheki.

 “Kagasheki tumemuondoa kwa vile ni waziri na sehemu ya serikali, hivyo tumebakia madiwani 15,” alisema.

 Hata hivyo, inajulikana kuwa hata Kagasheki anawaunga mkono itakapofika hatua ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya.

 Gaspar aliongozana na madiwani wenzake watatu wa Viti Maalumu, Rabia Badru (CUF), Murungi Kichwabuta (CCM) na Winfrida Mukono wa CHADEMA.

 Aliwataja madiwani wengine waliosaini barua hiyo kutoka CCM kuwa ni Alexander Ngalinda wa Kata ya Buhembe ambaye pia ni Naibu Meya, Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).

 Kwa CHADEMA madiwani wote wanne, Dismas Rutagwelela wa Kata ya Rwamisenyi, Israel Mlaki (Kibeta), Conchester Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalumu na Mukono wamesaini huku watatu wa CUF, Ibrahim Mabruk wa Kata ya Bilele, Felician Bigambo (Bakoba) na Rabia nao wakisaini hati hiyo.

 Madiwani hao wamesisitiza kwamba wanaweza kumaliza suala hili wenyewe bila rais kuhusishwa.

 Walisema kuwa hawapingi miradi hiyo bali hawakubaliani na namna meya anavyotaka kuiendesha kifisadi bila kuwashirikisha.

Chimbuko la mgogoro

CHADEMA kupitia kwa viongozi wake wa Wilaya ya Bukoba Mjini wakiwemo madiwani wake wanne, ndio waasisi halisi wa hoja za kupinga miradi ya kifisadi iliyoingiwa na Amani pasipo kufuata utaratibu wa kisheria.

 Kupitia uhamasishaji wa mikutano ya hadhara, viongozi hao waliwaelimisha wananchi kuhusu hasara itakayotokana na utekelezaji wa miradi hiyo, japo walipata upinzani mkubwa kutoka kwa meya na madiwani wa CCM.

 Awali, wakati CHADEMA wakitoa shutuma hizo dhidi ya meya, Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Kagasheki na Meya Amani lao lilikuwa moja. Wote walitamba hadharani kwamba miradi hiyo lazima itekelezwe.

 Hata hivyo, kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, katika moja ya vikao vya Baraza la Madiwani, mbunge alishtuka baada ya kubaini kwamba hoja za CHADEMA zilikuwa za kweli, na kwamba miradi inayosimamiwa na meya itawaletea wakazi wa Bukoba maumivu  ya muda mrefu mbele ya safari.

 Alimpinga meya hadharani, hata akaitisha mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa pia na meya Amani; akasema yeye kama mbunge hawezi kukubaliana nae katika miradi ya kifisadi.

 Hatimaye, madiwani wengine wanane wa CCM wakaona hoja ya mbunge ina mantiki; na baada ya kutaka maelezo yenye mantiki wakayakosa, wakashawishi wenzao wa CUF kusaini azimio la kumwondoa meya.

 Hata hivyo, baada ya Kagasheki kuibeba hoja ya CHADEMA akiungana na madiwani wengine wa CCM na CUF, alihitaji kuungwa mkono na madiwani wanne wa CHADEMA ili kukamilisha akidi inayoweza kupiga kura ya kumwondoa meya.

 Kwa kugundua hilo, meya naye anadaiwa kuingilia ngome ya CHADEMA, ili kuwagawa na kupunguza kura.

 Baada ya muda mfupi, wakati shinikizo la kumwondoa meya likiwa limepamba moto, uongozi wa CHADEMA Manispaa ulikaa na wabunge wake katika kikao ambacho kiliisha kwa mgawanyiko.

 Madiwani wawili wa CHADEMA, Rutagwelera (Rwamishenyi) na Mulaki (Kibeta), waliingia kikaoni wakiwa na msimamo wa kukataa katakata kupiga kura ya kumwondoa meya, kwa kigezo kuwa hiyo hoja si yao bali ya CCM.

 Kwa sababu hiyo, madiwani wawili waliobaki, Rwamlaza na Mukono, waliendelea kushikilia msimamo wa awali, kwamba meya aondoke, jambo ambalo liligeuzwa na kutumiwa kipropaganda kuwachafua ndani ya chama kwamba wamehongwa na Kagasheki.

 Kundi la Rwamlaza na Mukono linaamini kwamba wao ndio waasisi wa hoja ya ufisadi wa meya, na kwamba wangekuwa watu wa ajabu kuachana nayo eti kwa vile imeungwa mkono na madiwani wa CCM.

 Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa CHADEMA walianza kukosana mara baada ya Kagasheki kukaa na baadhi yao kujadili hoja za kumwondoa meya, huku baadhi yao wakiwatuhumu wenzao kwamba mbunge huyo amewahonga; na wao wakituhumu wenzao waliotaka kumnusuru meya, kwamba wamehongwa ili kura za kumwondoa zisitoshe.

 Hata hivyo, katika uamuzi wa jana hata wale madiwani wawili wa CHADEMA waliokuwa wamegomea uamuzi wa kumwondoa meya walisaini barua; hali inayoonyesha wamerudi katika msimamo wa awali wa wapambanaji wa ufisadi ndani ya halmashauri hiyo.

 Meya na mashabiki wake wamekuwa wakitaka kugeuza mgogoro wa maslahi ya umma uonekane ni mgogoro binafsi kati yake na mbunge. Baadhi yao wamekuwa wakidiriki hata kushutumu gazeti hili kwa kuweka hadharani habari hizi, na hata kudiriki kulituhumu kuwa linahongwa na Kagasheki.

 Propaganda hizi zilifikia mahali zikaingizwa hata katika uongozi wa CHADEMA Bukoba Mjini kiasi cha kuwagawa katika makundi mawili; moja likitaka meya aondoke, jingine likitaka abaki kwa maelezo kuwa huu ni ugomvi binafsi kati ya Kagasheki na Amani.

 Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa uongozi wa wilaya na mkoa unamtetea meya, na taarifa alizopewa rais kuhusu mgogoro huo zimelenga kufunika funika mambo ili CCM isiaibike, lakini umeshindwa kuwadhibiti wanaompinga kwa sababu ni kweli miradi hiyo ina ufisadi na haikufuata utaratibu.

 Kikwete hakuwa wa kwanza kujaribu kufunika kombe. Kabla yake CCM Taifa ililazimika kuingilia kati. Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Philipo Mangula, alifika Bukoba Februari mwaka huu, na kukutana na uongozi wa CCM wilaya wakiwemo madiwani na kuwaagiza waondoe tuhuma zao dhidi ya meya akidai walikiuka utaratibu.

 Hatua hiyo ilizidi kukuza mgogoro, na hivyo Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye kulazimika kuingilia kati kwa kuiomba Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuunda tume ya kuchunguza tuhuma hizo.

 Tume hiyo iliundwa na kwenda Bukoba kuchunguza tuhuma hizo, lakini haijawekwa hadharani; na kauli ya rais ililenga kufunika ugunduzi wa tume hiyo.

 Wadadisi wa mambo wanasema Rais Kikwete hakutarajiwa amalize mgogoro huu kwa sababu si tabia ya CCM kukemea ufisadi katika serikali kuu au halmashauri zake.

 Lengo lao lilikuwa kuzuia hatua zozote ambazo zingechukuliwa dhidi ya meya, hasa kwa kuwa mbunge naye amejiunga na kambi ya madiwani wanaotaka awajibishwe.

 Juzi Rais Kikwete aliagiza kuwa kabla ujenzi huo wa soko haujaanza, wahakikishe wananchi wanapatiwa eneo mbadala ambalo litakuwa la muda kwa ajili ya kuendelea na biashara zao wakati wakisubiri kukamilika kwa ujenzi.

 Alisema wafanyabiashara wa soko hilo wasiharibiwe maisha yao hata kama wapo kwenye soko la zamani, bado wanapata riziki zao katika soko hilo.

 Rais aliagiza kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo wafanyabiashara waliokuwepo awali ndio wapewe kipaumbele katika soko jipya.

 Pia aliagiza halmashauri hiyo kuwagawia viwanja 800 wananchi waliokuwa wamelipa fedha kwa ajili ya kupimiwa mwaka 2003 kwa sh 50,000 hadi 70,000 kutoka katika mradi wa viwanja 5,000 wa sasa bila kuwatoza nyongeza ya fedha ya ziada.

 Maagizo ya rais ndiyo hasa yamekuwa sehemu ya hoja za wanaotaka meya awajibike.

 Kwa miaka mitatu mfululizo CHADEMA imekuwa ikisimamia hoja hiyo na kumtaka meya asitishe miradi, afuate taratibu na atende haki kwa wahusika wote – wakazi wa Bukoba na wafanyabishara watakaoguswa na utekelezaji wa miradi hiyo.

No comments:

Post a Comment