RAIS Jakaya Kikwete ameshindwa kutanzua mgogoro wa ufisadi wa
miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, badala
yake amejielekeza kuwataka Meya Anatory Amani na Mbunge, Balozi Khamis
Kagasheki, kumaliza tofauti zao.
Kauli yake imepingwa vikali na baadhi ya madiwani wakidai kuwa
kiongozi huyo hafahamu kwa undani kiini cha mgogoro husika kuwa ni
masilahi ya wananchi.
Juzi akihutubia mkutano katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Rais
Kikwete alisema ujenzi wa soko kuu la kisasa katika manispaa hiyo lazima
uendelee na kwamba hakuna hoja ya kuendelea na malumbano yasiyokuwa na
msingi.
Alisema kuwa mbunge na meya wakiendelea kutiliana shaka wanaoumizwa ni
wananchi, hivyo kuwaagiza viongozi hao kumaliza tofauti zao kwa kile
alichodai hakuna lisilokuwa na mwisho.
Wakizungumza na gazeti hili jana kwa masharti ya kutotajwa majina yao,
baadhi ya madiwani hao walieleza kushangazwa na kauli ya rais kuwa
mgogoro huo ni jambo dogo.
Wakizungumza kwa hisia kali walisema kuwa hoja si ugomvi kati ya meya
na Kagasheki bali hawakubaliani na jinsi meya huyo anavyotaka kuendesha
miradi hiyo mitatu kifisadi.
Madiwani hao wa CCM walidai kuwa rais amepotoshwa kwa kuelezwa kwamba
mgogoro huo ni baina ya Amani na Balozi Kagasheki wakati hoja hiyo
iliasisiwa na madiwani wa CHADEMA kisha mbunge wao na madiwani wengine
kuunga mkono.
“Shida yetu si kupinga miradi hiyo mitatu ya ujenzi wa soko la kisasa,
kituo cha mabasi wala upimaji na ugawaji wa viwanja. Tatizo ni jinsi
meya anavyotaka kuendesha miradi hiyo kifisadi bila kutushirikisha sisi
kama wawakilishi wa wananchi.
“Wakati wenzetu wa CHADEMA wanaanza kupinga utekelezwaji wa miradi hii
tuliwabeza na kudhani ni mambo ya kisiasa, lakini baadaye tukabaini
kwamba meya anatuuza, hivyo baadhi yetu akiwamo Kagasheki tuliamua
kuwaunga mkono,” walisema.
Madiwani hao walisisitiza kuwa mgogoro huo hauwezi kumalizwa kienyeji
kiasi ambacho Rais Kikwete anataka bila meya Amani kuachia ngazi.
“Hapa Bukoba wananchi hawana imani tena na meya, huyu ana masilahi
yake binafsi na anakumbatiwa na baadhi ya viongozi wa CCM na serikali
wanaonufaika naye, hivyo msimamo wetu uko pale pale lazima ang’oke ndipo
miradi iendelee,” alisema diwani mmoja.
Katika kuonesha kukasirishwa na msimamo wa rais, madiwani hao walisema
kuwa leo watawasilisha barua yao kwa mkurugenzi wa manispaa ili kumtaka
aitishe kikao cha kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya.
“Rais anasema haya ni mambo madogo ambayo hayapaswi kufika kwake. Huyu
ni kiongozi wa aina gani asiyefuatilia mgogoro huu wa dhuluma kwa
wananchi wake? Hana taarifa kama CCM imepoteza wafuasi kwa sababu ya
meya?” alihoji diwani mwingine.
Chimbuko la mgogoro
CHADEMA kupitia kwa viongozi wake wa Wilaya ya Bukoba Mjini wakiwamo
madiwani wake wanne, ndio waliasisi hoja za kupinga miradi ya kifisadi
iliyoingiwa na Amani pasipo kufuata utaratibu wa kisheria.
Kupitia uhamasishaji wa mikutano ya hadhara, viongozi hao
waliwaelimisha wananchi kuhusu hasara itakayotokana na utekelezaji wa
miradi hiyo, japo walipata upinzani mkubwa kutoka kwa meya na madiwani
wa CCM.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh
bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhama ya Uwekezaji (UTT) haukufuata
taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha
malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata
utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB)
bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye
kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini
hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh
milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa
mapato na matumizi ya mradi wa kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa
kituo cha mabasi.
Awali, wakati CHADEMA wakitoa shutuma hizo dhidi ya meya, Mbunge wa
Bukoba Mjini, Balozi Kagasheki na Meya Amani lao lilikuwa moja. Wote
walitamba hadharani kwamba miradi hiyo lazima itekelezwe.
Hata hivyo, kuelekea mwishoni mwa mwaka jana, katika moja ya vikao vya
Baraza la Madiwani, mbunge alishtuka baada ya kubaini kwamba hoja za
CHADEMA zilikuwa za kweli, na kwamba miradi inayosimamiwa na meya
itawaletea wakazi wa Bukoba maumivu ya muda mrefu mbele ya safari.
Alimpinga meya hadharani, hata akaitisha mkutano wa hadhara ambao
ulihudhuriwa pia na Meya Amani; akasema yeye kama mbunge hawezi
kukubaliana na meya katika miradi ya kifisadi.
Hatimaye, madiwani wengine wanane wa CCM wakaona hoja ya mbunge ina
mantiki; na baada ya kutaka maelezo yenye mantiki wakayakosa,
wakashawishi wenzao wa CUF kusaini azimio la kumwondoa meya.
Madiwani hao ni Alexander Ngalinda (Buhembe), ambaye pia ni naibu
meya; Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM wa wilaya,
Richard Gaspar (Miembeni), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga) na Robert
Katunzi (Hamugembe).
Wengine ni Dauda Kalumuna (Ijuganyondo), Ibrahim Mabruk (Bilele), Rabia Badru na Murungi Kichwabuta wa Viti Maalumu.
Hata hivyo, baada ya Kagasheki kuibeba hoja ya CHADEMA akiungana na
madiwani wengine wa CCM na CUF, alihitaji kuungwa mkono na madiwani
wanne wa CHADEMA ili kukamilisha akidi inayoweza kupiga kura ya
kumwondoa meya.
Kwa kugundua hilo, meya naye anadaiwa kuingilia ngome ya CHADEMA ili kuwagawa na kupunguza kura.
Baada ya muda mfupi, wakati shinikizo la kumwondoa meya likiwa
limepamba moto, uongozi wa CHADEMA manispaa ulikaa na wabunge wake
katika kikao ambacho kiliisha kwa mgawanyiko.
Madiwani wawili wa CHADEMA, Dismas Rutagwelera (Rwamishenyi) na Israel
Mulaki (Kibeta), waliingia kikaoni wakiwa na msimamo wa kukataa
katakata kupiga kura ya kumwondoa meya, kwa kigezo kuwa hiyo hoja si yao
bali ya CCM.
Kwa sababu hiyo, madiwani wawili waliobaki, Conchesta Rwamlaza na
Winfrida Mukono, waliendelea kushikilia msimamo wa awali, kwamba meya
aondoke.
Kundi la Rwamlaza na Mukono linaamini kwamba wao ndio waasisi wa hoja
ya ufisadi wa meya, na kwamba wangekuwa watu wa ajabu kuachana nayo eti
kwa vile imeungwa mkono na madiwani wa CCM.
Wakati hali ikiwa hivyo CHADEMA, uamuzi huo wa madiwani uliigawa pia
CCM na kuonekana kama ugomvi kati ya Kagasheki na Amani. Kutokana na
mpasuko kuwa mkali CCM taifa ililazimika kuingilia kati.
Makamu Mwenyekiti wa CCM taifa, Philip Mangula, alifika Bukoba
Februari mwaka huu na kukutana na uongozi wa CCM wilaya wakiwamo
madiwani na kuwaagiza waondoe tuhuma zao dhidi ya meya, akidai walikiuka
utaratibu.
Hatua hiyo ilizidi kukuza mgogoro, hivyo Katibu wa Itikadi na Uenezi
taifa, Nape Nnauye, kulazimika kuingilia kati kwa kuiomba Wizara ya
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuunda tume ya kuchunguza tuhuma
hizo.
Tume hiyo iliundwa na kwenda Bukoba kuchunguza tuhuma hizo ingawa hadi
Rais Kikwete anawataka meya na mbunge wamalize tofauti zao ripoti bado
haijatolewa.
Rais Kikwete aliagiza kuwa kabla ujenzi huo wa soko haujaanza
wahakikishe wananchi wanapatiwa eneo mbadala ambalo litakuwa la muda
kwa ajili ya kuendelea na shughuli zao za biashara wakati
wakisubiri kukamilika kwa ujenzi.
Alisema wafanyabiashara wa soko hilo wasiharibiwe maisha yao, hata
kama wapo kwenye soko la zamani bado wapate riziki zao katika soko hilo.
Kwamba, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo,
wafanyabiashara waliokuwepo awali ndio wapewe kipaumbele katika soko
jipya.
Pia aliagiza Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kuwagawia viwanja 800
wananchi waliokuwa wamelipa fedha kwa ajili ya kupimiwa viwanja mwaka
2003 kwa sh 50,000 hadi sh 70,000 kutoka katika mradi wa viwanja 5,000
wa sasa bila kuwatoza nyongeza ya fedha ya ziada.
Alihoji ni kwa nini wananchi hao hawakupewa viwanja wakati wamelipa na
hata baada ya kukosa viwanja ilikuwaje wasirudishiwe fedha zao.
Aliwata halmashauri kujihesabu kuwa wao ndio waliochelewa kuwapa
wananchi viwanja hivyo, kwamba wawapatie sasa, fidia watajua wenyewe
jinsi ya kufidia kiasi cha fedha kinachohitajika.
No comments:
Post a Comment