Tuesday, July 30, 2013

ASASI YA KULEA YATIMA YAISAIDIA SERIKALI KATIKA MAPAMBANO YA KIPINDUPINDU



Na Ibrahim Yassin,Kyela

KUFUATIA ongezeko la mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kuzidi kuongezeka wilayani Kyela mkoani Mbeya asasi ya The Mango Tree inayojishughulisha na kulea watoto yatima imetoa msaada wa dawa za kutibu maji kwa wakazi wa kata sita ambazo zimeathirika zaidi na ugonjwa huo

Msaada huo umekwenda sambamba na kuwapatia watoto yatima vifaa vya kusomea kama Madaftari,kalamu,pencils,Free Style kwa watoto wa kike na vyandarua kwa ajiri ya kuwakinga na ugonjwa wa maralia ambao pia bado unawasumbua watu wengi wilayani Kyela

Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo katika kata za Bujonde na Ngonga kiongozi wa mpango huo kutoka katika asasi hiyo ya The Mango Tree Bw,Obed Helly alisema kuwa kama jamii itatumia vizuri dawa hizo za kutibu maji wana uhakika mkubwa wa kupunguza kasi ya ugonjwa huo wa kipindupindu

Alisema jamii inachotakiwa sasa ni kuhakikisha kuwa inazingatia kanuni za afya ikiwa ni pamoja na kuzitumia dawa hizo ipasavyo na kuwa kutumia dawa ni rahisi zaidi badala ya jamii kuchemsha maji na kuwa kila mmoja akitekeleza wajibu wake kila kitu kinawezekana

Mkuu wa idara ya elimu katika asasi hiyo Bw,Aloyce  Mwakapotela alidai kuwa ipo haja kwa walezi wanaowalea watoto yatima kuhakikisha kuwa wanavitunza vifaa hivyo wanavyopewa ili viweze kuwasaidia watoto hao na kuwawezesha kupata elimu kama ilivyo kwa watoto wengine

Taarifa za idara ya afya zinaonyesha kuwa ugonjwa wa kipindupindu bado ni tatizo kwa maana kuwa idadi ya wagonjwa wapya imekua ikiongezeka siku hadi siku ambapo mpaka sasa wagonjwa waliopo ni 112 na huenda hari hiyo ikaendelea kutokana na ukaidi wa watu kutofuata kanuni za afya kama wanavyoelekezwa na wataalamu wa afya

Kaimu mganga mkuu wa wilaya Kyela Bi,Apaisaria Rumisha amesema kuwa kama wananchi wataziunga mkono jitihada za serikali za kupambana na ugonjwa huo kuna matumaini makubwa ya kuweza kuondokana na tatizo hilo lakini kama hari itaendelea hivyo basi tatizo hilo litaendelea kuisumbua wilaya Kyela

Kutokana na hari hiyo serikali ya wilaya imezuia mikusanyiko mbalimbali ya watu isiyokuwa ya lazima,uuzaji wa vyakula na vyakula kutouzwa kwenye maeneo ya shule za msingi na sekondari na mpaka sasa kuna baadhi ya watu wamekamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa makosa mbalimbali ya kukiuka sheria za kupambana na ugonjwa huo
MWISHO

No comments:

Post a Comment