Thursday, March 14, 2013

MIMBA MASHULENI TAKUKURU LUDEWA WATU 92 WAHOJIWA KUBAINI TATIZO.



  Na Bazil Makungu
          Ludewa

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru)katika Wilaya ya Ludewa imehoji wadau wa elimu zaidi ya 60 katika utafiti wake wa kubaini rushwa za mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Akitoa taarifa ya utafiti katika warsha ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo mkuu wa taasisi hiyo wilaya Edings Mwakambonja alisema ofisi yake iliamua kufanya utafiti huo kama njia ya kuwanusuru watoto wa kike ambao wamekuwa wakitelekezwa baada ya kupata mimba kwa wazazi kunufaika kwa kulipana na wahalifu.

Mwakamboja aliwaambia washiriki wa warsha hiyo kuwa madhumuni ya utafiti wake ni kubaini mianya ya rushwa katika kesi za mimba kwa wanafunzi wa sekondari katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa.

Pamoja na kubaini pia mianya ya rushwa kwa watendaji wa vijiji, kata na walimu wakuu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na kuwalinda watuhumiwa wanaohusika na kuwapa wanafunzi mimba.

Mwakambonja akaongeza kuwa ofisi yake ilitaka kubaini pia endapo wazazi na wanafunzi wanaopata mimba wanapokea hongo kutoka kwa watuhumiwa ili wasichukuliwe hatua za kisheria na kubaini kama endapo sheria, kanuni na sera za elimu kama zinafuatwa ili kuwawajibisha wahusika.

Aidha mwakambonja alieleza eneo la utafiti na namna alivyopata sampuli kuwa ni pamoja na kuhoji jumla ya watu 92 wakiwemo wanafunzi 40, wananchi 20, mkuu wa polisi wilaya ya Ludewa (OCD) na afisa elimu sekondari.

Wengine ni waratibu kata 9 maafisa watendaji kata 9 maafisa watendaji wa vijiji 12 na kwamba nia ya kuwahoji wadau hao ni kupata taarifa za msingi na kuzingatia miongozo na sera mbalimbali za elimu ili kukusanya na kuthibitisha uzingativu wa sera na miongozo hiyo.

MWAKAMBONJA matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba watuhumiwa wanaowapa wanafunzi mimba hutoa hongo kwa watendaji na wazazi wa wanafunzi ili kukwepa vyombo vya dola kwa kufanya usuluhishi.

Akitoa ufafanuzi Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Ludewa Fredrick Lukuna kuna haja ya kuwa na mashine za kupimia (DNA) kila wilaya ili kurahisisha na kubaini ukweli mapema kuliko ilivyo sasa ambapo watu wamekuwa wakifuata huduma hiyo jijini Dar es salaam ambako ni gharama.

Alisema ni kutokana na kipimo hicho kuwa mbali ndiyo maana wazazi wamekuwa mstari wa mbele katika kukubali kulipana kwa kigezo kuwa mtuhumiwa akifungwa atawaachia mzigo wa kulea vijukuu.

,,, wakuu wa shule wamekuwa wakitoa taarifa kwa watendaji kata lakini hawafanyi ufuatiliaji kuona ni hatua zipi za kisheria zimechukuliwa kwa watuhumiwa waliohusika na uhalifu wa kuwapa wanafunzi wao mimba.,,,, akalaumu Lukuna

Kaimu afisa elimu sekondari Gelda Ng’asi akaongeza kuwa katika kuthibiti mimba na rushwa mashuleni kuna haja ya wananchi/jamii na wazazi wenyewe kushirikiana na kuunganisha nguvu zao na kuamua kukataa mimba za wanafunzi katika maeneo na vijiji vyao.

Hata hivyo akaongeza kuwa ili kuondoa tatizo la mimba mashuleni kuna haja ya wanafunzi wenyewe kupewa elimu na kufanya kampeni ya kujitambua ili wajue athari za mimba shuleni lakini pia sheria zirekebishwe kwa maana ya kutoa adhabu sawa kwa wavulana na wasichana hiyo inaweza kujenga hofu.

Wilaya ya Ludea ina jumla ya shule za sekondari 21 zikiwemo za bweni na kutwa na kati ya hizo shule 18 ni mali ya serikali na 3 zinamilikiwa na taasisi binafsi, wadau wa elimu wamelalamkia shule hizo kuwa watuhumiwa wamekuwa hawachukuliwi hatua za kisheria kutokana na kuendekeza rushwa.

No comments:

Post a Comment