MGOGORO wa vizimba katika soko la wafanyabiashara wadogo la
Machinga Complex lililoko jijini Dar es Salaam umeingia hatua nyingine
baada ya Meneja wa soko hilo, Nyamsukura Masondore kuvamiwa na
wafanyabishara hao, kumpiga hadi kumvunja mkono.
Tukio hilo lilitokea Januari 7, mwaka huu, wakati
Meneja huyo akiwa ziarani kuhakiki umiliki halisi wa mpangaji na ulipaji
wa kodi kwa vizimba hivyo.
Akiwa katika mahojiano na Mwananchi, Msondore
alisema kuwa wakati wa zoezi hilo la kuhakiki wapangaji na walipakodi
ghafla alivamiwa na watu wasiopungua wanane na kumpiga hadi kumvunja
mkono.
“Nilikuwa nimeongozana na viongozi wenzangu kwenye
shughuli hiyo ya uhakiki, ghafla nikavamiwa na watu ambao wanadaiwa ni
wafanyabiashara wa hapa kwenye jengo na wengine wa Soko la Karume
wakanipiga hadi kunivunja mkono,” alisema Masondore.
Masondore alisema kuwa alitoa taarifa katika Kituo
cha Polisi cha Pangani katika Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam na
kupewa RB ya polisi no Ila/rb/75/2013 kwa kosa la shambulio la kudhuru
mwili, na uchunguzi wa polisi unaendelea.
Aliongeza kuwa kutokana na tukio hilo alishindwa
kuendelea na uhakiki huo wa vizimba na walipakodi na kuelekea Hospitali
ya Amana iliyopo Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam ambapo ndipo
anapata matibabu hadi sasa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha
Minangi Komba alisema kuwa hana taarifa za kutokea kwa vurugu hizo
katika jengo hilo la wafanyabiashara wadogo.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa
Wafanyabiashara wa jengo hilo, Abubakari Rakesh ameulalamikia uongozi wa
jengo kuwa tangu kuzinduliwa kwa gulio lililopo ndani ya jengo hakuna
ufuatiliaji wowote uliofanyika ili kuutaka kujua maendeleo ya
wafanyabiashara.
Alisema kuwa uzinduzi huo ambao ulifanywa na Naibu
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Abdalah Chaurembo haukuwa wazi
kwa kila mtu jambo ambalo halikupangwa kufanyika hivyo tangu taratibu
hizo za uzinduzi zianze.
“ Uzinduzi huu ulikuwa wa kimyakimya jambo ambalo
hatukupanga hivyo, tulitegemea matangazo mbalimbali yawekwe kwa ajili ya
kuwakumbusha wafanyabiashara na wananchi pia juu ya uzinduzi, lakini
haukufanyika hivyo, naweza kusema ulikuwa uzinduzi wa funika kombe
mwanaharamu apite”, alisema Rakeshi.
Rakesh aliongeza kuwa uongozi wa jengo hilo
ulitakiwa uwe mstari wa mbele kwa ajili ya kutetea maslahi ya
wafanyabiashara wanaofanya biashara zao hapo lakini badala yake uongozi
huo haupo bega kwa bega na wafanyabiashara hao.
No comments:
Post a Comment